Na mwandishi wetu
Timu ya soka ya Red Arrows ya Zambia imeibuka kinara wa michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kombe la Kagame baada ya kuilaza APR ya Rwanda kwa penalti 10-9.
Ushindi wa Arrows umepatikana Jumapili hii jioni kwenye Uwanja wa KMC Dar es Salaam baada ya timu hizo kutoana jasho kwa dakika 90 pamoja na 30 za nyongeza zote kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Katika dakika 90 za kawaida, Arrows ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 72, ambalo lilifungwa na Ricky Banda kabla ya APR kusawazisha dakika ya 90 kwa bao lililofungwa na Mamadou Say.
Baada ya matokeo hayo timu hizo ziliingia kwenye dakika 30 za nyongeza lakini hadi dakika hizo zinamalizika hakuna timu iliyoliona lango la mwenzake na hatimaye kupigiana penalti.
Katika mikwaju ya penalti, Arrows walifanikiwa kufunga penalti zao 10 wakati APR walipata penalti tisa baada ya Arsene Tuyisenge kushindwa kuzifumania nyavu.
Katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu iliyochezwa awali, Al Hilal ilifanikiwa kushika nafasi hiyo ilipoilaza Hay Al Wadi kwa penalti 3-2 baada ya timu hizo ambazo zote za nchini Sudan kumaliza dakika 90 kwa sare ya bao 1-1.
Sambamba na kombe na medali, mshindi wa michuano hiyo inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) pia alizawadiwa kitita cha dola 30,000 wakati timu iliyoshika nafasi ya pili ilipewa dola 20,000 na ya tatu dola 10,000 pamoja na zawadi za fedha na medali kwa timu yenye, nidhamu, mfungaji bora, nyota wa mchezo na nyinginezo.
Kimataifa Red Arrows bingwa Kombe la Kagame
Red Arrows bingwa Kombe la Kagame
Related posts
Read also