Manchester, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amemkumbuka kocha wa muda wa timu hiyo, Ralf Rangnick (pichani) na kudai kwamba kocha huyo alikuwa sahihi kusema kwamba timu hiyo ilihitaji mabadiliko makubwa.
Rangnick aliyekuwa kocha kwa kipindi cha miezi saba aliifanisha timu hiyo na mtu ambaye anahitaji kufanyiwa ‘upasuaji wa moyo’ akimaanisha mabadiliko makubwa badala ya kugusa mambo madogo madogo ambayo hayawezi kumaliza tatizo.
Ten Hag alipewa majukumu ya kuinoa Man United mwaka 2022 baada ya Rangnick ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya taifa ya Austria kuinoa timu hiyo kwa kipindi cha miezi saba.
Akiwa kocha Man United, Rangnick hadi anaondoka timu hiyo aliiacha ikimaliza ligi katika nafasi ya sita ingawa aliiwezesha kushida mechi 11 kati ya 29 kabla ya Ten Hag kukabidhiwa majukumu.
Ten Hag, 54, ambaye hivi karibuni aliongeza mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo, amesisitiza kwamba Rangnick alikuwa sahihi katika tathmini yake.
“Hakika Rangnick alikuwa sahihi, tumekuwa tukifanya juhudi kubwa katika hili kwa kipindi cha miaka miwili lakini alichosema kilikuwa sahihi, ni mabadiliko kwa mapana na nilifahamu wakati naanza jambo hilo kwamba ingekuwa kazi ngumu,” alisema Ten Hag.
Man United imekuwa ikifanya mabadiliko makubwa ya kiuongozi kwa kubadili watendaji kuanzia Desemba mwaka jana mara baada ya bilionea wa Uingereza, Sir Jim Ratcliffe kununua asilimia 27 ya hisa katika klabu hiyo.
Kuhusu usajili wachezaji kadhaa wamesajiliwa na Ten Hag amethibitisha kuwa mshambuliaji Jadon Sancho ambaye aliingia katika utata na kocha huyo Agosti mwaka jana kabla ya kuuzwa kwa mkopo Baorussia Dortmund naye nafasi yake kwa sasa ipo kwenye kikosi cha Man United.
Katika kujiwinda na msimu mpya wa 2024-25 Man United imecheza mechi ya kitafiki na Rangers Jumamosi na kupata ushindi wa mabao 2-0, mabao hayo yakifungwa na Amad Diallo na Joe Hugill.