Miami, Marekani
Rais wa Shirikisho la Soka Colombia, Ramon Jesurun (pichani) na mtoto wake wa kiume, Ramon Jamil wamekamatwa na polisi kufuatia vurugu za Jumapili wakati wa mechi ya fainali ya Copa America dhidi ya Argentina.
Taarifa ya idara ya polisi wa Miami ilieleza kuwa Ramon, 71 na mwanawe Jamil, 43 wamekamatwa wakihusishwa na vurugu za kwenye mechi hiyo iliyoisha kwa Argentina kuilaza Colombia bao 1-0 na kubeba taji la Copa America.
Katika taarifa hiyo ilieleza kwamba makosa waliyoshtakiwa wawili hao yanahusisha vurugu zilizotokea uwanjani baada ya mechi ingawa Ramon na Jamil bado hawajasema lolote kuhusu mashtaka hayo.
Vurugu hizo zinadaiwa kufanywa baada ya kumalizika kwa mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Hard Rock ambapo Ramon na Jamil awali walikuwa wakielekea uwanjani lakini ghafla hali ilibadilika na kuonekana waliojawa hasira.
Katika hali ambayo haikutarajiwa, wawili hao hapo hapo walianza kuwapigia makelele maofisa usalama ambao walielekezwa kuwazuia watu kusogea zaidi eneo la uwanjani.
Mmoja wa maofisa usalama alionekana akimzuia Jamil kifuani na kumtaka asisogee zaidi eneo la uwanjani na ndipo vurugu zilipoanza baada ya Ramon kumsukuma ofisa huyo wakati huo Jamil naye akamkaba shingo ofisa huyo na kumuangusha chini kabla ya kuanza kumpiga mateke kichwani.
Baadaye Ramon naye alimkaba ofisa usalama mwanamke aliyekuwa akitoa msaada huku habari nyingine zikidai kwamba Ramon na mwanawe pia walimpiga ngumi meneja wa maofisa hao.
Habari nyingine zinadai kwamba Ramon na mwanawe walikuwa wakielekea kwenye eneo la uwanja kwa ajili ya kushiriki katika hafla ya utoaji tuzo kabla ya kuingia katika tafrani hiyo.
Kimataifa Rais wa soka Colombia akamatwa
Rais wa soka Colombia akamatwa
Read also