Na mwandishi wetu
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameagiza klabu za soka ambazo hazina viwanja vilivyo katika ubora utakaoidhinishwa na Shirikisho la Soka Tanania (TFF) ziwekwe pembeni.
Kiongozi huyo wa serikali, ametoa agizo hilo Jumatatu hii wakati wa hafla ya uzinduzi wa mtambo wa Teknolojia ya VAR iliyoandaliwa na Kampuni ya Azam Media na kufanyika katika viwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Akisitiza umuhimu wa viwanja bora, Waziri Mkuu aliwataka TFF kuwapa masharti wanachama wao wanaomiliki viwanja na atakayeshindwa kutimiza masharti hayo awekwe pembeni
Alisema kwamba Tanzania inahitaji kufika mbali kwenye viwango vya ubora Afrika na kutaka washindane na nchi za Misri na Morocco ambazo zimepiga hatua kubwa katika ubora barani Afrika.
Waziri Mkuu alisema serikali imeipa kipaumbele michezo na hilo linadhihirishwa na namna ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa mchango wake katika sekta hiyo na kuondoa ile dhana ya Tanzania kichwa cha mwendawazimu.
Akiizungumzia teknolojia ya VAR alisema kwamba itasaidia kupunguza malalamiko kwa timu pamoja na kupunguza makosa ya kibinadamu kwa waaamuzi na kuwafanya wawe makini katika kazi yao.
Teknolojia ya VAR au Video Assistance Referee hutumika kwa lengo la kumsaidia mwamuzi kujiridhisha na maamuzi hasa yale yenye utata kwa kuyarejea kupitia picha za video za mechi husika.
Teknolojia hiyo ambayo imekuwa ikitumika katika Ligi Kuu England (EPL), Kombe la Dunia 2018 na 2022 na Euro 2024 hata hivyo imekuwa ikilalamikiwa kwa kuchelewesha kutoa maamuzi na hata maamuzi yake wakati mwingine kuonekana yamejaa utata.
Ni hivi karibuni tu katika fainali za soka za Euro 2024 nchini Ujerumani, kocha wa Uholanzi, Ronald Koeman alisema kwamba VAR inaua soka.
Soka Majaliwa: Klabu zisizo na viwanja bora zitengwe
Majaliwa: Klabu zisizo na viwanja bora zitengwe
Read also