Dortmund, Ujerumani
England imeilaza Uholanzi mabao 2-1 na sasa itaumana na Hispania Jumapili ijayo kwenye dimba la Olimpiki katika mechi ya fainali Euro 2024, mechi ambayo mshindi atakuwa bingwa wa fainali hizo.
Ushindi wa England katika mechi hiyo ya nusu fainali iliyopigwa Jumatano hii unaifanya timu hiyo kusogea hatua zaidi katika mbio za kuliwania taji hilo ililolikosa mwaka 2020 baada ya kulala mbele ya Italia kwa mikwaju ya penalti katika mechi ya fainali.
Uholanzi ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao mapema dakika ya saba Xavi Simons, kabla ya Harry Kane kusawazisha kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 18.
England ilipambana kwa hali na mali na kukawa na kila dalili kwamba timu hizo zingeenda katika dakika 30 za nyongeza lakini Ollie Witson aliyeingia akitokea benchi alibadili matokeo katika dakika ya 90 na kuipeleka England katika hatua ya fainali.
Hii sasa itakuwa mechi ya tatu kwa England dhidi ya Hispania kwenye fainali za Euro ikikumbukwa kuwa katika mechi mbili zilizopita England iliibuka na ushindi mara zote na swali ni je safari hii Hispania itakubali kuendeleza uteja wake kwa England?
Mwaka 1980 England iliifunga Hispania mabao 2-1 katika hatua ya makundi, fainali zilizopigwa nchini Italia na mwaka 1996, England ikiwa nyumbani katika Euro 96 iliitoa Hispania kwa mikwaju ya penalti katika hatua ya mtoano.
Kimataifa Ni England, Hispania fainali Euro 2024
Ni England, Hispania fainali Euro 2024
Read also