Manchester, England
Klabu ya Manchester United inadaiwa kuongeza ofa ya kumsajili beki kisiki wa klabu ya Everton, Jarrad Branthwaite (pichani) baada ya ofa yao ya awali ya Pauni 35 milioni kukataliwa mwezi uliopita.
Jarrad ambaye pia ni beki wa kimataifa wa England amekuwa akiwindwa na Man United na sasa timu hiyo ipo tayari kutoa Pauni 45 milioni na malipo mengine ya ziada kama malengo yatafikiwa.
Everton wamekuwa wagumu kumuachia kiurahisi beki huyo ambaye yuko katika kiwango bora na hadi sasa klabu hiyo haijaweka wazi msimamo wake kama watakubali kiasi hicho cha fedha au la.
Katika msimu uliopita wa Ligi Kuu England (EPL) wa 2023-24, Jarred alitoa mchango mkubwa kwa timu hiyo na kuisaidia isishuke daraja licha ya kunyang’anywa pointi mbili baada ya kukutwa na hatia ya kukiuka kanuni za matumizi ya fedha.
Man United imepania kuimarisha safu yake ya ulinzi ambapo mbali na Jarred pia inaifukuzia saini ya beki wa Bayern Munich, Matthijs de Ligt ambaye kwa sasa anaiwakilisha Uholanzi kwenye fainali za soka za Euro 2024 zinazoendelea nchini Ujerumani.
Juhudi za Man United kuimarisha kikosi chake zinaendelea ikiwa tayari imeondokewa na Raphael Varane wakati huo huo majaliwa ya beki wa kati wa timu hiyo, Jony Evans yakiwa njia panda kuhusu kuongezewa mkataba wa mwaka mmoja.
Mchezaji mwingine ambaye majaliwa yake Man United yapo njia panda ni Victor Lindelof ambaye licha ya kuwa tayari ameripoti katika kambi ya timu hiyo lakini huenda akaachana nayo wakati wowote.
Kimataifa Man United yampandia dau beki wa Everton
Man United yampandia dau beki wa Everton
Read also