Na mwandishi wetu
Simba imewaeleza wazi mashabiki wake kuwa wanapaswa kufurahi kutokana na usajili unaoendelea kufanyika katika kikosi hicho kwani ni usajili wa kitaalam mno.
Mpaka leo Jumapili Simba imetambulisha jumla ya wachezaji tisa wapya kwa ajili ya msimu mpya wa 2023-24.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula amefafanua kuwa timu hiyo iliendelea na usajili mkubwa hata kabla ya kuwa na kocha mkuu kutokana na matunda ya timu kubwa ya skauti na wachambuzi wa kikosi chao.
Kutokana na hilo Kajula amewataka wapenzi wa Simba kutokuwa na wasiwasi kwani maskauti hao ndio waliomshusha mchezaji bra wa Ligi Kuu Ivory Coast, Ahoua Charles kwa ajili ya manufaa ya Simba msimu ujao.
“Niwaeleze tu kwamba timu kubwa iliyopo ya wachambuzi wa kikosi, mchezaji, mahitaji ya timu ndio imekuja na ripoti ya kueleza timu inataka nini kulingana na msimu uliopita.
“Kisha sasa maskauti wanaingia mbali zaidi kutazama mahitaji ya timu na wachezaji wanaohitajika huku pia ukitazama mikataba ya wanaomaliza na unafanyaje ili kuendana na ripoti ya kujenga timu,” alifafanua Kajula.
Alisema kwa jinsi Simba inavyosukwa na timu nyingine zinavyotengeneza timu zao ni dhahiri inaonesha ubora mkubwa wa Ligi Kuu Bara, akiwataka si tu Wanasimba kujivunia hilo bali Tanzania kwa ujumla.
Ukiachana na Clatous Chama aliyetimkia Yanga, Simba imewapa mkono wa kwaheri aliyekuwa nahodha wao, John Bocco, Kennedy Juma, Saido Ntibazonkiza, Henock Inonga, Shaban Chilunda na Luis Miquissone.
Wachezaji wapya ni Lameck Lawi, Joshua Mutale, Steven Mukwala, Abdulrazack Hamza, Valentino Mashaka, Augustine Okajepha, Debora Mavambo, Omari Omari na Ahoua.
Timu hiyo ipo kwenye mchakato mkubwa wa kusuka kikosi kitakachorejesha makali yao baada ya kulikosa taji la ligi kuu kwa misimu mitatu sasa wakilishuhudia taji hilo likitua Yanga.
Juzi Simba imemtangaza pia mrithi wa Abdelhak Benchika, Fadlu Davis raia wa Afrika Kusini aliyetua na jopo lake la benchi la ufundi, tayari kuipeleka Simba katika nchi ya ahadi.
Msimu ujao timu hiyo itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika ambako itahitaji kuonesha ubabe wake kutokana na kiwango ilichokuwa ikionesha kwenye Ligi ya Mabingwa kwa misimu minne mfululizo, hivyo inajipanga kuhakikisha hilo linatimia.
Agosti 3, mwaka huu Simba itafanya tamasha lake la kila mwaka la Simba Day kuonesha vifaa vyao vipya walivyosajili kwa ajili ya michuano mbalimbali watakayoshiriki msimu ujao.