Berlin, Ujerumani
Umoja wa Vyama vya Soka Ulaya (Uefa) unachunguza tukio la kiungo wa timu ya taifa ya England, Jude Bellingham kutoa ishara isiyopendeza kwenye soka wakati wa mechi ya hatua ya mtoano dhidi ya Slovakia.
Bellingham ambaye ndiye aliyefunga bao la kusawazisha katika mechi hiyo ya fainali za Euro 2024 iliyopigwa juzi Jumapili na England kushinda 2-1 anadaiwa kutoa ishara ya kushika koo na kuelekezea kwenye benchi la Slovakia wakati akishangilia bao hilo.
Kutokana na tukio hilo Uefa sasa inachunguza tukio hilo na huenda ikamchukulia hatua mchezaji huyo kwa kosa la kufanya kitendo ambacho ni kinyume na ustaarabu wa soka.
Bellingham hata hivyo alikana kwamba kitendo alichokifanya kilikuwa na lengo la kuwadhihaki Slovakia badala yake alisema kwamba ni utani ambao aliuelekeza kwa marafiki zake wa karibu.
Ikitokea Uefa kumkuta na hatia mchezaji huyo ambaye ndio kwanza amefikisha umri wa miaka 21, inaweza kumpa adhabu ya kumfungia kucheza mechi kadhaa, kumpiga faini au vyote viwili.
“Ilikuwa ni utani kwa marafiki wa karibu ambao walikuwa uwanjani, vinginevyo sina jingine zaidi ya kuwaheshimu Slovakia kwa namna walivyocheza mechi,” alisema Bellingham.
Kwa Bellingham si mara yake ya kwanza kuonesha ishara hiyo, aliwahi kufanya hivyo kwenye mechi ya Real Madrid, lakini pia alifanya hivyo hivyo alipofunga bao kwenye mechi ya kirafiki ya England dhidi ya Ubelgiji miezi kadhaa iliyopita.
Mwaka 2019, Cristiano Ronaldo akiwa Juventus alitozwa faini ingawa hakufungiwa mechi hata moja baada ya kukutwa na hatia ya kutoa ishara ya aina hiyo alipofunga bao katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Atletico Madrid.