Gelsenkirchen, Ujerumani
Nahodha wa timu ya taifa ya England, Harry Kane amempongeza kiungo wa timu hiyo, Jude Bellingham kwa bao alililofunga dhidi ya Slovakia katika mechi ya mtoano ya fainali za Euro 2024 zinazoendelea nchini Ujerumani.
Bellingham alifunga bao kwa staili ya tikitaka jana Jumapili katika mechi ambayo England ilitoka uwanjani na ushindi wa mabao 2-1 hivyo kufuzu hatua ya robo fainali na Jumamosi itacheza dhidi ya Switzerland.
Kane alisema kwamba mafanikio hayo yalitokana na tamaa na shauku waliyokuwa nayo na kila mmoja aliyehusika kwenye timu ingawa anakiri kwamba hali ilikuwa ngumu lakini waliendelea kupambana.
“Tulifanyia kazi kila kitu kwa kipindi cha wiki nzima, kwa siku kadhaa tulifanyia kazi mambo mengi ambayo tulisema yatahitajika, tulilazimika kuwa tayari kwa kila kitu, na hicho ndicho ambacho Jude alikifanya, ni goli ambalo huwezi kuamini, ni kati ya magoli bora katika historia ya nchi yetu,” alisema Kane.
Kane alisema kwamba Bellingham ni mchezaji wa ana yake anayefanya juhudi kubwa kwa ajili ya timu na baada ya mengi kuzungumzwa kuhusu yeye katika siku za karibuni hatimaye ameonesha anachoweza kukifanya katika tukio kubwa.
“Tulijua kwamba tutafanya kila kilichohitajika, kama tutakuwa na mechi kama hii kwenye robo fainali na iwe tu hivyo, ni lazima tupambane na hicho ndicho tulichofanya, tungeweza kufanya vizuri zaidi lakini mwisho wa siku ni matokeo ndiyo yanayoangaliwa, hivyo tuna kila sababu ya kufurahia na kuendelea na kasi hii kwenye fainali hizi,” alisema Kane.
Katika mechi hiyo, Slovakia ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 25 lililofungwa na Ivan Schranz na kuibua wasiwasi kwamba huenda huo ungekuwa mwisho wa England kwenye fainali hizo baada ya Slovakia kulilinda vyema bao lao.
Bellingham hata hivyo aliiokoa England kwa bao hilo kali katika dakika tano za nyongeza, bao ambalo lilizifanya timu hizo kumaliza dakika 90 zikiwa sare na hivyo kuongezewa dakika 30 ambazo England ilizitumia vyema kupata bao la pili lililofungwa na Kane.
Ukiachana na bao la Bellingham ambalo limeonekana kuwa gumzo kutokana na ubora wake, baadhi ya wachambuzi bado wana hofu na kiwango cha England kama itaweza kufanya vyema kwenye robo fainali.
Katika mechi nyingine ya hatua ya mtoano, Hispania iliibugiza Georgia mabao 4-1 na hivyo kufuzu kibabe hatua ya robo fainali ambapo katika hatua hiyo itakutana na wenyeji Ujerumani hapo Ijumaa.
Matokeo mechi za mtoano Euro 2024
England 2-1 Slovakia
Hispania 4-1 Georgia
Mechi za mtoano Euro 2024 leo Jumatatu
Ufaransa vs Ubelgiji
Ureno vs Slovenia