Dortmund, Ujerumani
Kocha wa Denmark, Kasper Hjulmand (pichani) amekerwa na matumizi ya VAR ambayo anaamini ndiyo yaliyoiwezesha Ujeumani kupata ushindi wa mabao 2-0 katika mechi ya mtoano ya fainali za Euro 2024 zinazoendelea Ujerumani.
Kasper amelalamikia VAR akidai kuwa kwa kipindi kisichozidi dakika mbili maamuzi ya VAR yameinyonga timu yake na kuwabeba wenyeji ambao sasa wanasubiri kucheza robo fainali.
Mwamuzi wa mechi hiyo, Michael Oliver alilikataa bao la Joachim Anderson wa Denmark katika dakika ya 48 baada ya VAR kubaini kuwa kiungo wa Denmark Thomas Delaney alikuwa kwenye aneo la kuotea
Dakika mbili baadaye mwamuzi huyo aliwapa penalti Ujerumani baada ya maofisa wanaosimamia VAR, kumtaka apitie upya tukio lililohusisha Anderson kuunawa mpira wa krosi ya David Raum na hatimaye kuipa penalti Ujerumani.
Kai Havert akapiga vyema mkwaju wa penalti uliokwenda moja kwa moja wavuni kabla ya Jamal Musiala kuiongezea Ujerumani bao la pili baadaye.
“Ni mechi iliyoamuliwa kwa matumizi ya VAR mara mbili, nina picha hapa inayomuonesha Delaney kuotea, ni sentimita moja, haileti mantiki yoyote, hivi sivyo tunavyotakiwa kutumia VAR,” alisema Hjulmand.
“Na dakika chache baadaye Ujerumani wanapata penalti, nimechoka na maamuzi haya, hatuhitaji tena kuwa na beki atakayecheza kwa kutumia mikono kama hivi, Anderson alikuwa akikmbia, ni mazingira ya kawaida na alipigwa na mpira akiwa mita kadhaa,” alisema Hjulmand.
Hjulmand alisema ni mara chache mno yeye kuzungumzia waamuzi lakini ilikuwa muhimu kwa mechi hiyo kwani kama wangekuwa mbele kwa bao 1-0 pia ingeweza kubadili kila kitu katika mechi hiyo,
Kocha hyo hata hivyo pamoja na malalamiko hayo aliipongeza Ujerumani kwa ushindi na kuitakia heri lakini akasisitiza kwamba hivyo sivyo mpira unavyoendeshwa.
Matokeo mechi za mtoano Euro 2024
Switzerland 2-0 Italia
Ujerumani 2-0 Denmark
Mechi za mtoano Euro 2024 leo Jumapili
England vs Slovakia
Hispania vs Georgia