Munich, Ujerumani
Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya England, Wayne Rooney amesema kiungo wa timu hiyo, Jude Bellingham anaonekana kama amevurugwa kwenye fainali za soka za Euro 2024 zinazoendelea nchini Ujerumani.
England imefuzu hatua ya mtoano ya fainali hizo ikiwa kinara Kundi C lakini kiwango cha timu hiyo hakijawavutia wengi, imeshinda mechi moja tu dhidi ya Serbia kwa bao 1-0, bao hilo pekee mfungaji akiwa ni Bellingham.
Baada ya mechi hiyo, Bellingham, 20 ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Real Maddrid ya Hispania, hakuweza kuonesha kiwango cha juu katika mechi dhidi ya Denmark na Slovenia.
“Jude alianza vizuri mechi ya kwanza lakini nina hakika hata yeye anaweza kukwambia kwamba hakuwa katika ubora wake kwenye mechi mbili za mwisho,” alisema Rooney ambaye kwa sasa ni kocha na mchambuzi.
Rooney ambaye pia ni mshambuliaji wa zamani wa England, alisema anamuona Bellingham ni kama amevurugwa na hata yeye (Rooney) aliwahi kujikuta katika mazingira ya aina hiyo na hata katika mechi jana (juzi) Bellingham alionesha hali hiyo.
“Yote hiyo inaonesha kwamba hayuko vizuri katika michuano hii, anajitoa kwa asilimia 100 na sidhani kama kwenye hilo kuna tatizo, anataka wachezaji wenzake wajitoe zaidi na nafikiri hicho ndicho anachokipigania,” alisema Rooney.
Rooney alisema kwamba anachokisema si kwamba anatoa shutuma bali kwa upande mwingine inaweza kuwa ni kumpa sapoti ni kwa kuwa isije ikafika pahala akajikuta akivurugwa hadi kupewa kadi nyekundu kipuuzi.
England ambayo Jumapili itacheza na Slovakia katika hatua ya mtoano, imeshutumiwa kwa kiwango duni na wanasoka wa zamani ambao kwa sasa ni wachambuzi, Gary Lineker, Micah Richards na Alan Shearer.