Na mwandishi wetu
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limeifutia klabu ya Yanga adhabu ya kufungiwa kusajili wahezaji baada ya kumlipa aliyekuwa mchezaji wao, Lazarus Kambole (pichani).
Taarifa ya TFF iliyopatikana Jumatano hii ikiwa imesainiwa na ofisa habari na mawasiliano wa shirikisho hilo, Cliford Ndimbo ilieleza kuwa mchezaji huyo aliwasilisha malalamiko yake Fifa akiilalamikia klabu hiyo kwa kutomlipa ujira wake.
Kwa mujibu wa taarifa ya TFF, Kambole alishinda kesi hiyo na Yanga ambao ni vinara wa Ligi Kuu NBC msimu wa 2023-34 walitakiwa kumlipa ndani ya siku 45 lakini hawakufanya hivyo kwa wakati.
Baada ya Yanga kushindwa kutekeleza uamuzi huo wa Fifa, uamuzi wa kuifungia klabu hiyo kufanya usajili ulitangazwa na TFF hivi karibuni ikiwa ni kutekeleza hukumu hiyo ya Fifa.
Taarifa ya TFF hata hivyo haikutaja kiasi cha fedha ambazo Yanga ilikuwa ikidaiwa na mchezaji huyo raia wa Zambia badala yake ilieleza kuwa klabu hiyo imefutiwa adhabu ya kutosajili kwa kuwa tayari imemlipa Kambole haki zake.
Wakati huo huo TFF imetangaza kozi ya maboresho kwa makocha wakuu na wasaidizi wa timu za Ligi Kuu NBC na wale wa timu za taifa, kozi ambayo imepangwa kufanyika Julai 15 mkoani Tanga ambapo kila mshiriki atatakiwa kulipa ada ya shilingi 500,000.
Soka Fifa yaifutia Yanga adhabu
Fifa yaifutia Yanga adhabu
Read also