Stuttgart, Ujerumani
Kiungo wa timu ya taifa ya Ubelgiji, Kevin De Bruyne amewataka mashabiki wa timu hiyo wenye hasira kuipa sapoti timu hiyo baada ya kuwazomea wakichukizwa na sare ya 0-0 dhidi ya Ukraine jana Jumatano.
Ubelgiji hata hivyo imefuzu hatua ya mtoano kwenye Euro 2024 na Jumapili itaikabili Ufaransa mjini Dusseldorf, mechi ambayo itaamua timu ipi iende robo fainali na De Bruyne amewataka mashabiki kuwaunga mkono katika mechi hiyo.
Mashabiki wa Ubelgiji pamoja na kufahamu kwamba timu yao imefuzu hatua ya mtoano lakini waliwazomea wachezaji kwa kuwa walitaka timu hiyo ishinde ili iwe kinara Kundi E.
Awali De Bruyne alijaribu kukabiliana na mashabiki hao lakini baadaye akaachana nao na kuwataka wachezaji wenzake waondoke baada ya zomeazomea kuongezekana wakati mchezji huyo akitajwa kuwa nyota wa mchezo huo.
“Tulijaribu kushinda mechi, tulikuwa na nafasi za kufunga magoli lakini hatukuwa tayari kujiweka katika mazingira hatarishi hasa katika mipira ya kona kwa sababu tulijua tungeweza kufungwa,” alisema De Bruyne.
De Bruyne hata hivyo alikiri kwamba ni aibu kwao kutofunga magoli kwa kuwa walikuwa na nafasi za kufanya hivyo na hali inapokuwa hivyo wanachohitaji ni mashabiki kuwa nao pamoja.
“Hawa mashabiki tunawahitaji, tutawahitaji katika mechi dhidi ya Ufaransa, hilo ndilo jambo pekee ninaloweza kulisema,” alisema De Bruyne.
Alipoulizwa ni kwanini aliwaambia wachezaji wenzake waondoke uwanjani na si kuzungumza na mshabiki wa Ubelgiji, De Bruyne aliishia kusisitiza umuhimu wa mashabiki katika timu yao kwenye mechi dhidi ya Ufaransa.
Ratiba ya mechi za mtoano Euro 2024
Switzerland v Italia (Jumamosi Juni, 29)
Ujeruman v Denmark (Jumamosi Juni, 29)
England v Slovakia (Jumapili Juni, 30)
Hispania v Georgia (Jumapili Juni 30)
Ufaransa v Ubelgiji (Jumatatu Julai 1)
Portugal v Slovenia (Jumatatu Julai 1)
Romania v Uholanzi (Jumanne Julai 2)
Austria v Uturuki (Jumanne Julai 2)