Cologne, Ujerumani
Kiwango duni cha England kwenye Euro 2024 nchini Ujerumani kimewakera mashabiki wake hadi kuwazomea na kuwarushia makopo wachezaji na kocha wao jana Jumanne katika mechi yao na Slovenia iliyoisha kwa sare ya 0-0.
Zomeazomea hiyo imemshangaza kocha wa timu hiyo, Gareth Southgate ambaye ametaka mashabiki kuiunga mkono timu hiyo ambayo imemaliza Kundi C ikiwa inashika usukani na kufuzu hatua ya mtoano.
Katika mechi hiyo, England ilipiga mashuti manne tu yaliyolenga goli jambo lililowakera mashabiki lakini Southgate amesisitiza kwamba mashabiki wanatakiwa kuiunga mkono timu hiyo.
Timu hiyo ilikutana na zomeazomea hiyo wakati wa mapumziko na hata baada ya mpira kumalizika Southgate alipowasogelea mashabiki na kuwaonesha ishara ya kuwashukuru wapo waliomuunga mkono na wengine kutomuunga mkono waziwazi.
Southgate hata hivyo aliwatetea wachezaji wake akitaka wasizomewe badala yake alisema kwamba anaweza kuelewa hali hiyo ikielekezwa kwake.
“Naweza kuelewa mtazamo wao kwangu na hiyo ni afadhali kuliko kuelekeza mtazamo wao kwa wachezaji inaleta mazingira tata kwenye timu, sijawahi kuona timu yoyote inafuzu na kujikuta katika hali kama hii,” alisema Southgate.
Southgate hata hivyo alisema kwamba ataendelea kuwashukuru mashabiki ambao wanakuwa watu wazuri kwake wakati wote wa mchezo.
Hatma ya Southgate kuendelea kukinoa kikosi cha England itajulikana mara baada ya fainali za Euro 2024 kumalizika ingawa mkataba wake na timu hiyo unafikia mwisho Desemba mwaka huu.
Matokeo Euro 2024 jana Jumanne
Kundi C
England 0-0 Slovenia
Denmark 0-0 Serbia
Kundi D
Uholanzi 2-3 Austria
Ufaransa 1-1 Poland