Na mwandishi wetu
Azam FC imeeleza kuwa itaanza rasmi mawindo yake ya msimu ujao kuanzia Julai 6 kabla ya kupaa kwenda Morocco Julai 14, mwaka huu kwa lengo la kukamilisha maandalizi hayo.
Hayo yameelezwa leo Jumanne na meneja habari na mawasiliano wa Azam, Thabiti Zakaria ambapo amefafanua kuanzia Julai Mosi watakuwa wakipokea wachezaji kabla ya Julai 5 kuanza rasmi kujifua Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
“Tutafanya mazoezi Azam Complex mpaka tarehe sita kabla ya kuondoka tarehe saba kwenda Zanzibar ambapo pia tutaanza kujifua tarehe saba hiyo hiyo mpaka tarehe 13.
“Baada ya hapo tutarejea Dar es Salaam na tarehe 14 tutaondoka kwenda Morocco kwa ajili ya kambi ndefu na tutakuwa huko hadi mwisho wa mwezi wa saba na kisha kurudi Dar kufungua msimu rasmi tukianza na Ngao ga Jamii,” alisema Zakaria.
Azam imeeleza kuwa inahitaji maandalizi kabambe kuelekea msimu ujao kutokana na malengo waliyonayo ya kufanya vizuri kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya msimu uliomalizika hivi karibuni kumaliza katika nafasi ya pili katika Ligi Kuu NBC, nyuma ya mabingwa Yanga SC.