Na Hassan Kingu
Simba imeachana na kiungo wake, Saido Ntibazonkiza ambaye habari za kuachwa kwake zimewekwa wazi kwenye mitandao ya kijamii katika siku za hivi karibuni.
Baadhi yetu tayari tulilitambua hilo mapema hasa kwa jinsi baadhi ya mashabiki walivyoanza kumzungumzia vibaya mchezaji huyo kabla hata ya uamuzi wa kuachana naye kufikiwa.
Uamuzi wa Simba hata hivyo haumaanishi kuwa Ntibazonkiza amefikia mwisho wa maisha yake ya soka, hapana, bado ana nafasi ya kuendelea kucheza soka tena la ushindani, iwe hapa Tanzania au nje ya Tanzania.
Sina uhakika na timu za nje lakini kwa hapa Tanzania naiona nafasi yake katika kikosi cha Coastal Union, naiona nafasi hiyo hiyo pia katika kikosi cha Azam FC.
Timu zote hizo mbili msimu ujao wa 2024-25 zitashiriki michuano ya klabu barani Afrika, Azam watashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Coastal watashiriki Kombe la Shirikisho Afrika kama ilivyo kwa Yanga.
Michuano hii ni mikubwa na sitoshangaa baadhi ya timu za hapa Tanzania zikiaga mapema kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, kwa mantiki hiyo suala la kuimarisha vikosi kwa kuongza nguvu ni jambo muhimu.
Azam wamelitambua hilo na tayari wameanza na hapana shaka wanaendelea kukiimarisha kikosi chao, Coastal nao wanatakiwa kufanya hivyo na kwangu mtu wa kwanza ambaye wanaweza kumchukua ni Ntibazonkiza.
Ni mchezaji mbunifu ambaye anaweza kuongeza kitu katika eneo la kiungo, amedhihirisha hilo akiwa Simba na nadhani kwa Coastal anaweza kuwa mpishi mzuri na ambaye ataipa nguvu safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Coastal wasione ajabu kumchukua Ntibazonkiza eti kwa kuwa ameachwa na Simba badala yake waangalie mahitaji ya kikosi chao, Yanga na Simba si mara moja wamekuwa wakiacha wachezaji na kuchukuliwa upande wa pili.
Mfano wa karibuni ni kwa Jonas Mkude ambaye Simba walimuacha Yanga wakamsajili, hivyo haitokuwa ajabu Coastal kumchukua Ntibazonkiza kutokana na mahitaji ya timu na hata uwezo wao kiuchumi.
Nasema hivyo kwa sababu Coastal wanaenda kwenye mashindano magumu yanahitaji aina ya wachezaji wabunifu, wazoefu ambao wana uwezo wa kubadili matokeo.
Nimewahi kusema huko nyuma kwamba Ntibazonkiza ni aina ya mchezaji ambaye anaweza kuingia uwanjani muda ambao timu pinzani imeamua kupaki basi na akasaidia kubadili matokeo kutokana na aina ya uchezaji wake wa kujiamini ikibidi hata kupiga chenga kufungua vyumba.
Ninachokiona ni kwamba hadi sasa Coastal bado hawajafanya usajili wowote unaoendana na hadhi ya timu inayojiandaa kushindana katika mashindano ya klabu barani Afrika, badala yake tulichosikia ni kwamba beki wao amehamia Simba.
Kwangu mimi naona Ntibazonkiza ni mmoja wa wachezaji wenye hadhi si ya Ligi Kuu NBC na michuano mingine ya ndani bali hata michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hivyo anaweza na ana sifa zote za kuisaidia timu hiyo.
Bado sioni tatizo au ubaya wowote kwa Coastal kukiongezea nguvu kikosi chake kwa kumsajili Ntibazonkiza, naamini wakifanya uamuzi huo hawawezi kujuta.
Najua wapo wanaoweza kushangaa ninapomtaja Ntibazonkiza na kumhusisha na Azam, tusishangae hoja yake inasimamia maandalizi ya timu kwenye Ligi ya Mabingwa, hata ni mashindano makubwa ambayo timu shiriki inatakiwa iwe imekamilika kila idara.
Msimu uliopita, Azam ililalamikiwa mara kwa mara kwa kukosa kipa mzuri, hilo wamelifanyia kazi, Mustapha Mohamed unaweza kumtaja kuwa kipa mwenye hadhi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, anaweza kuwa msaada na hata akipatakana aliye bora zaidi yake ni vizuri zaidi.
Ni hivi karibuni tu Azam wametudhihirishia udhaifu wao kwenye mikwaju wa penalti hadi kushindwa kutamba mbele ya Yanga kwenye Kombe la Shirikisho CRDB, walioangalia mechi ile hadi kwenye penalti watakubaliana na mimi.
Sasa kama kweli wanakwenda Ligi ya Mabingwa na hawataki udhaifu wowote kwenye timu yao basi kwenye penalti, Ntibazonkiza ni chaguo sahihi.
Hili nalo linaweza kushangaza wengi na kuhoji yaani asajiliwe kwa ajili ya penalti tu au mipira ya adhabu, hapana Ntibazonkiza ana sifa nyingine kama ambavyo nimezieleza hapo juu lakini hili la penalti nalo si la kupuuza hata kidogo, si udhaifu wa kuachwa kama una uwezo ni vyema kuuziba.
Katika Ligi ya Mabingwa linapozungumziwa suala la timu kuwa kamili maana yake ni kutoupa nafasi udhaifu wowote kwenye timu na kuingia nao katika mashindano hayo, kufanya hivyo ni kujiruhusu kushindwa. Una tatizo la penalti, tafuta wapiga penalti kabisa.
Udhaifu huu wa penalti upo hadi Yanga, kitendo cha kupigiana penalti hadi tisa na Azam maana yake ni kwamba kuna tatizo katika eneo hilo na wanahitaji kulifanyia kazi kama kweli wanahitaji kuwa washindani kwenye Ligi ya Mabingwa.
Tena Yanga ndio wanatakiwa kuliangalia hili kwa macho mapana zaidi kwani wameshindwa kuweka historia ya kufikia nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa kukosa wapiga penalti wazuri, nao wanatakiwa kujiandaa na hilo vinginevyo watakwama tena.
Sisemi wamsajili Ntibazonkiza lakini wanatakiwa kukubali kilicho wazi kwamba penalti ni mtihani kwao, walifanyie kazi hilo hasa kwa kuwa anayesajiliwa hasajiliwi ili apige penalti tu bali anakuwa na sifa nyingine za ziada kama ilivyo kwa Ntibazonkiza.
Makala Namuona Ntibazonkiza, Coastal, Azam
Namuona Ntibazonkiza, Coastal, Azam
Read also