Munich, Ujerumani
Kocha wa Uholanzi, Ronald Koeman amesema mwamuzi alikosea kulikataa goli lao katika mechi dhidi ya Ufaransa kwenye fainali za soka za Kombe la Ulaya ‘Euro 2024’ zinazoendelea nchini Ujerumani.
Ufaransa ikicheza bila nahodha wake Kylian Mbappe jana Ijumaa ililazimishwa sare ya 0-0 na Uholanzi, matokeo ambayo hata hivyo Koeman alisema yamefurahiwa na timu zote baada ya kugawana pointi moja moja.
Bao la Uholanzi lililofungwa kipindi cha pili na Xavi Simons lilikataliwa kwa kuwa Denzel Dumfries alikuwa eneo la kuotea karibu na kipa Mike Maignan ambapo pia VAR ilitumika na uamuzi kufikiwa baada ya muda mrefu.
Koeman hata hivyo alisema kwamba baadaye aliangalia tukio lile kwenye picha na katika hoja yake akasema hakubaliani na uamuzi wa mwamuzi wa mechi hiyo, Anthony Taylor wa England.
“Ndio alipokuwa Dumfries ni eneo la kuotea, ni kweli lakini hakumsumbua kipa na hali inapokuwa hivyo kwa maoni yangu goli linakuwa halali,” alisema Koeman.
Koeman pia alihoji kama ni kweli zilihitajika dakika tano za kuangalia VAR huku akisisitiza kwamba alichokiona ni kwamba mchezaji hakumsumbua kipa.
Naye nahodha wa Uholanzi, Virgil van Diyk alisema kwamba goli lingeachwa kama lilivyo kwa kuwa lilikuwa halali.
Matokeo hayo yanaonekana kuwaacha katika wakati mgumu Ufaransa hasa kwa kuwa hawajui hatma ya Mbappe, mshambuliaji wao mahiri aliyeumia pua ambaye walitarajia angecheza mechi dhidi ya Uholanzi hiyo jana lakini hali imekuwa tofauti.