Atlanta, Marekani
Ushindi wa mabao 2-0 ilioupata Argentina dhidi ya Canada kwenye Copa America unatoa dalili za timu hiyo kubeba taji la tatu kubwa mfululizo baada ya Copa America 2021, Kombe la Dunia 2022 na sasa inataka tena Copa America 2024.
Ijumaa hii kwenye dimba la Mercedes-Benz nchini Marekani, nahodha wa Argentina, Lionel Messi aliiongoza vyema timu hiyo kuanza mbio za kulitetea taji hilo ambalo huenda timu yake ikalibeba kwa mara nyingine.
Kwa Messi ambaye Jumatatu alifikisha umri wa miaka 37 hiyo inakuwa mechi yake ya 35 kwenye fainali za Copa America na hivyo kumzidi mechi moja, Sergio Livingtone wa Chile.
Katika mechi hiyo Messi ndiye aliyekuwa mpishi wa bao la kwanza la Argentina baada ya kutoa pasi ya kichwa iliyomkuta Alexis Mac Allister kabla ya Alvarez kumalizia kazi ya kuujaza mpira wavuni.
Bao la pili la Argentina lilifungwa na Martinez na kwa mara nyingine lilitokana na mchango wa Messi aliyeunasa mpira katika eneo la kati la uwanja kabla ya kutoa pasi kwa mfungaji.
Baada ya ushindi huo, Argentina itajitupa uwanjani kwa mara nyingine Jumanne kuumana na Chile na kumalizia mzunguko wa kwanza kwa kuumana na Peru wakati Jumanne Canada itaumana na Peru kabla ya kumalizia mzunguko wa kwanza kwa kuivaa Chile.
Kimataifa Argentina yasaka taji la tatu
Argentina yasaka taji la tatu
Read also