Na mwandishi wetu
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imepanda kwa nafasi tano katika viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) na sasa inashikilia nafasi ya 114.
Katika viwango hivyo vilivyotolewa Alhamisi hii, Tanzania imeongezeka alama kutoka 1,160 ilizokuwa nazo mwezi Aprili mpaka alama 1,175 ilizovuna hadi Juni, mwaka huu.
Tangu mwezi Mei, Stars imeumana na Sudan katika mechi mbili za kirafiki ugenini ambapo ilifungwa mabao 2-1 kisha ikashinda bao 1-0.
Juni 2, timu hiyo ilicheza na Indonesia mchezo wa kirafiki ugenini ulioisha kwa suluhu kabla ya Juni 11 kuitandika Zambia bao 1-0 kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola, katika mechi ya Kundi E kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026.
Katika viwango hivyo kwa nchi za Afrika, Morocco imeendelea kuwa ya kwanza na ya 12 kidunia, ikifuatiwa na Senegal inayoshika nafasi ya 18 kidunia na ya tatu ni Misri inayokamata nafasi ya 36.
Wanaokamilisha 10 bora Afrika na nafasi zao kwenye mabano kidunia ni Ivory Coast (37), Nigeria (38), Tunisia (41), Algeria (44), Cameroon (49), Mali (50) na Afrika Kusini (59).
Kwa ujumla Argentina imeendelea kuwa ya kwanza, ikifuatiwa na Ufaransa, Ubelgiji, Brazil, England, Ureno Uholanzi, Hispania, Croatia na Italia inafunga dimba la 10 bora.
Kimataifa Tanzania yapanda viwango Fifa
Tanzania yapanda viwango Fifa
Read also