Hamburg, Ujerumani
Serbia imetishia kujitoa katika fainali za soka za Euro 2024 zinazoendelea Ujeumani kama Umoja wa Vyama vya Soka Ulaya (Uefa) hautochukua hatua dhidi ya udhalilishaji unaofanywa na mashabiki dhidi ya timu yao.
Tukio la zomeazomea zilizoandamana na kauli za dhihaka zilizoelekezwa na mashabiki dhidi ya Serbia zilisikika wakati wa mechi ya Albania na Croatia iliyopigwa mjini Hamburg na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Serbia, Jovan Surbatovic amesema kwamba Serbia haitokuwa tayari kuendelea na fainali hizo kama Uefa haitotoa adhabu stahiki kwa mashabiki hao.
Serbia ambao walitoka sare ya bao 1-1 na Slovenia katika mechi yao ya Kundi C iliyopigwa mjini Munich lakini katika hali ambayo haikutarajiwa walijikuta wakizomewa na kudhihakiwa wakati wa mechi ya Croatia na Albania.
“Kinachoendelea ni kashfa na tutaitaka Uefa itoe adhabu hata kama itabidi kutoendelea na fainali hizi, tutataka Uefa itoe adhabu kwa mashirikisho ya soka ya pande zote husika,” alisema Surbatovic.
Juzi Jumatano, Uefa ilimnyang’anya kadi ya kuripoti fainali za Euro 2024 mwandishi mmoja baada ya kudaiwa kutoa ishara ya kuwadhihaki mashabiki wa Serbia wakati wa mechi yao dhidi ya England iliyochezwa Jumapili iliyopita.