Munich, Ujerumani
Nahodha na mashambuliaji tegemeo wa timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappé amelazimika kukimbizwa hospitali baada ya kuumia pua katika mechi ya fainali za Euro 2024 dhidi ya Austria.
Ufaransa katika mechi hiyo ilitoka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 lakini kuumia kwa Mbappe kumeibua hofu licha ya baadaye kuelezwa kwamba mchezaji huyo hatohitaji kufanyiwa upasuaji.
Akiwatoa wasiwasi mashabiki wa Ufaransa, rais wa shirikisho la soka la nchi hiyo, Philippe Diallo alisema madaktari baada ya uchunguzi wamebaini kuwa Mbappe atakuwa sawa bila ya upasuaji.
Ufaransa baada ya mechi hiyo ya jana Jumatatu, itakuwa na mtihani mgumu Ijumaa ijayo katika mechi yake ya pili ya fainali hizo zinazoendelea nchini Ujerumani itakapowakabili Uholanzi.
Mbappe ambaye alihusika katika bao hilo pekee la Ufaransa aliumia baada ya kugongana na Kevin Danso wa Austria na hapo hapo akaanza kulalamika akimtaka kipa wa Austria, Patrick Pentz kuwaita watu wa huduma ya kwanza.
Baada ya tukio hilo, Mbappe alipatiwa matibabu na sehemu ya jezi yake ilionekana ikiwa na damu na ingawa alijaribu kuendelea kucheza lakini muda mfupi baadaye alijiangusha chini huku akiwa ameshika uso.
Kujiangusha kwa Mbappe kuliwakera mashabiki wa Austria walioanza kumzomea wakiamini ilikuwa ni janja ya kupoteza muda ili kuinusuru Ufaransa isifungwe bao la kusawazisha na mwamuzi alimpa kadi ya njano lakini baadaye alitolewa na nafasi yake kuingia Olivier Giroud.
“Amepata maumivu ya pua, tutalazimika kusubiri ili kujua itakuwaje, timu ya madaktari inakabiliana na tatizo, tunalazimika kuangalia kinachoendelea na kujua itachukua muda gani, ni habari mbaya mno kwetu usiku wa leo,” alisema kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps.
Ufaransa ilineemeka na bao hilo pekee la dakika ya 38 ambalo Maximilian Wobe alijifunga na hivyo kuizawadia ushindi Ufaransa ambao unakuwa ushindi wa 100 kwa Deschamps akiwa na timu hiyo.