Manchester, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amesema akiwa katika mapumziko yake kwenye fukwe za Ibiza ghafla mabosi wa klabu hiyo walimfuata na kumwambia wanataka aendelee kuwa kocha wa timu hiyo.
Majaliwa ya Ten Hag katika kikosi cha Man United yamekuwa njia panda kabla na hata baada ya Man United kucheza mechi ya fainali ya Kombe la FA Mei 25 dhidi ya Man City na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Akizungumzia alivyofuatwa, Ten Hag alisema mabosi wa klabu hiyo walimfuata akiwa mapumzikoni Ibiza na hapo hapo baada ya kukutana naye wakamwambia wanataka aendelee na kazi akiwa na timu hiyo.
Man United imemaliza msimu wa 2023-24 wa Ligi Kuu England (EPL) ikiwa nafasi ya nane, nafasi ambayo ni ya chini mno katika kipindi cha miaka takriban 20 na hivyo habari za kutimuliwa kwa Ten Hag zikavuma kwa kasi kwenye vyombo vya habari.
Kabla ya kufuta mpango wa kumtimua, Ten Hag, mmiliki mwenza wa klabu hiyo, Sir Jim Ratcliffe alishafanya mazungumzo na aliyekuwa kocha wa Bayern Munich Thomas Tuchel ili akabidhiwe mikoba ya Ten Hag.
“Manchester United wameniambia kwamba walizungumza na Tuchel lakini mwishowe wakafikia hitimisho la kwamba tayari wana kocha bora,” alisema Ten Hag.
Alisema kwamba mabosi wa Ineos ambayo ni kampuni ya Sir Jim ni watu wapya katika soka kwa hiyo ilikuwa kawaida kwao kufanya tathmini ya msimu na si siri kwamba walifanya mazungumzo na makocha kadhaa.
Ten Hag hata hivyo alisema kwamba bado hajakaa na mabosi hao wa Man United kwa ajili ya kusaini mkataba mpya na kwamba jambo hilo watapata wasaa wa kulijadili.