Na Hassan Kingu
Moja ya mambo ambayo Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba aliyazungumza bungeni wakati akiwasilisha bajeti ya Serikali ni kuhusu matumizi ya VAR katika mechi za ligi kuu ya soka.
VAR au Video Assistance Referee ni teknolojia ambayo imekuwa ikitumika katika mechi za soka hasa Ligi Kuu England (EPL) pale panapokuwa na utata wa maamuzi ambapo mwamuzi hulazimika kujiridhisha kwa kutumia VAR.
Miongoni mwa matukio ambayo huwakanganya waamuzi na kujikuta katika wakati mgumu kufanya maamuzi ni matukio ya mchezaji kuotea, rafu, penalti, goli na mengineyo, mwamuzi anapoona hana uhakika na tukio husika hujiridhisha kwa kutumia VAR.
Kauli ya Waziri Nchemba kuhusu matumizi hayo inawezekana ikapokelewa vizuri na baadhi ya mashabiki wa soka lakini nadhani Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa wakati huu halina haja ya kuharakisha matumizi ya teknolojia hiyo.
Nasema hivyo kwa kuwa baadhi ya watu wenye heshima zao katika soka wanaamini teknolojia ya VAR imeshafeli na tayari kampeni za kuipiga vita zimeanza hasa England ambako hapo kabla iliaminika kuwa teknolojia hiyo ingekuwa mwarubaini wa matatizo mengi.
Kocha wa Tottenham Hotspur, Ange Postecoglou amewahi kunukuliwa akisema kwamba matumizi ya VAR yanafifisha nguvu za mamlaka ya mwamuzi katika matukio ya uwanjani na hivyo ni bora kuachana na teknolojia hiyo.
Ange alitoa kauli hiyo siku ambayo timu yake ilifungwa mabao 4-1 na Chelsea hapo hapo kukawa na matukio tisa ya kupitiwa kwenye VAR na hivyo kusababisha muda wa nyongeza kuwa mrefu baada ya dakika 90 za kawaida.
Katika mechi hiyo hiyo pia kulikuwa na matukio ya kukataliwa kwa mabao matano ambapo Ange alisema kwamba hapendi mambo ya kukaa na kusubiri muda mrefu kabla ya uamuzi sahihi kufikiwa.
Ange aliema amekuwa katika soka kwa miaka mingi na wakati wote amekuwa ni mtu wa kusubiri maamuzi yanayotolewa na mwamuzi, na katika hilo amekuwa akikutana na maamuzi ya kumuumiza na kumfurahisha.
Kocha huyo anaamini kuwa matumizi ya VAR ni ushahidi kwamba mwamuzi ameporwa mamlaka ya kuusimamia mchezo wa soka uwanjani badala yake mamlaka hayo sasa yanatoka nje.
Ange hata hivyo anakubaliana na ‘goal line technology’ kwa sababu ni jambo rahisi na lililo wazi lakini kwenye VAR kwa mapana yake ni kama vile imani kwa waamuzi haipo tena.
Mikel Arteta, kocha wa Arsenal naye amewahi kuilalamikia VAR baada ya timu yake kufungwa bao 1-0 na Newcastle katika mechi ya EPL, bao ambalo lilikubaliwa baada ya mapitio ya VAR.
Arteta alisema wazi kuwa bao hilo lilikuwa fedheha kubwa katika EPL na kujikuta akiingia matatani na mamlaka za soka England ingawa hakupewa adhabu yoyote.
Baadhi ya mashabiki Arsenal hadi sasa wanaamini matokeo ya mechi yao na Newcastle ambayo yalibebwa na matumizi ya VAR yalichangia pia kwa timu yao kulikosa taji la EPL.
Ni hivi karibuni tu klabu ya Wolverhampton Wanderers ilitangaza nia yake ya kuendesha kampeni kuzishawishi klabu za EPL kukataa matumizi ya VAR katika mechi zote za ligi msimu wa 2024-25.
Wolves, moja ya klabu ambazo zinadai kuumizwa na VAR inaamini matumizi ya teknolojia hiyo huwachanganya mashabiki na kuibua utata hasa kwa kuwa muda mrefu unatumika kuangalia VAR kabla ya kuja na majibu.
Kocha wa England, Gareth Southgate yeye alisema waziwazi kwamba hapendi matumizi ya VAR, na kuonesha jinsi alivyokerwa kuangalia mechi ya Chelsea na Spurs ambayo mashabiki mara kadhaa walitakiwa kusubiri VAR kwa ajili ya maamuzi.
Southgate alisema kwamba VAR imeharibu mechi hiyo maarufu London Derby kwa namna ambavyo mchezo umekuwa ukisimama mara kadhaa.
Kwa hiyo TFF nao wanatakiwa kuwa makini na ni vyema kujipa muda zaidi kabla ya kuamua kuhusu matumizi ya teknolojia ya VAR kwani huenda hayo ambayo tunayaona na kuyasikia EPL huku kwetu yakawa makubwa zaidi.
Kabla ya kuamua kuanza kutumia VAR, TFF ifanye tafakari isiharakishe, ijue tatizo likoje huko ilikoanza kutumiwa na kwa nini mambo yako hovyo kiasi cha kuanza kupigwa vita na watu mbalimbali wakiwamo makocha.
VAR awali ilionekana ingekuwa mwarubaini wa maamuzi tata uwanjani lakini kilichoonekana katika EPL ni kama teknolojia hiyo imeongeza utata, sasa ni muhimu kujiuliza hapa kwetu itakuwaje?
Soka Tanzania isiharakishe matumizi VAR
Tanzania isiharakishe matumizi VAR
Read also