Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Waziri Junior amelitoa bao lake pekee alilofunga jana Jumanne dhidi ya Zambia maalum kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Mbali na Rais Samia, mshambuliaji huyo wa klabu ya KMC, pia amelitoa bao hilo pekee katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola kwa familia yake na kwa kocha KMC, Abdulhamid Moallin.
“Kwangu nimefarijika sababu ndio mara ya kwanza nacheza mechi za kimafaifa kwenye michuano kama hii na nimefunga goli ambalo limeipa ushindi timu ya taifa kwa hiyo nimefurahi na namshukuru Mungu.
“Na goli nililofunga nalipeleka kwa watu watatu, wa kwanza ni Rais Mama Samia, wa pili ni famila yangu; mke wangu na mtoto wangu, na wa tatu ni Ahmed Moallin aliniambia ukifunga goli litakuwa goli langu kwa hiyo na yeye yumo katika watatu hao,” alisema Waziri.
Waziri aliyewahi kukipiga Yanga pia amefafanua kuwa katika mechi hiyo ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026, walikuwa na utulivu mkubwa kwani walipewa maelekezo na wachezaji wenye uzoefu mkubwa kama Himid Mao na Simon Msuva.
Kwa ushindi huo, Stars sasa imekuwa ya pili katika Kundi E kwa kufikisha pointi sita baada ya mechi tatu, kinara ni Morocco mwenye pointi tisa.
Niger inashika nafasi ya tatu ikiwa imekusanya pointi tatu kama ilivyo Zambia iliyo nafasi ya nne wakati Congo na Eritrea zikiburuza mkia bila pointi.
Stars inatarajia kurejea nchini kwa kutua Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam kesho Alhamisi majira ya saa 12 jioni.