New York, Marekani
Nahodha wa timu ya taifa ya Argentina na mshambuliaji wa Inter Miami FC ya Marekani, Lionel Messi, 36, amesema huenda Inter Miami ikawa timu yake ya mwisho kucheza soka la ushindani kwani anafikiri kustaafia hapo.
Messi ambaye ni mshindi wa tuzo za Ballon d’Or mara nane alijiunga na klabu hiyo ya Marekani majira ya kiangazi mwaka jana baada ya kuachana na PSG ya Ufaransa.
Kabla ya kujiunga na PSG, Messi alicheza kwa mafanikio na Barcelona ambapo alishinda mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mara nne pamoja na Ligi Kuu Hispania au La Liga mara 10.
Messi ambaye mwaka 2022 aliiwezesha Argentina kubeba Kombe la Dunia, mkataba wake wa sasa na Inter Miami unafikia okomo mwaka 2025 ingawa ana nafasi ya kuongeza mwaka mwingine mmoja.
“Nafikiri kwa wakati huu hii inaweza kuwa klabu yangu ya mwisho, japo sina mpango wa kuachana na soka moja kwa moja,” alisema Messi.
Kwa kiwango ambacho amekuwa akikionesha Messi haoneshi dalili zozote za kuelekea kustaafu, msimu huu amefunga mabao 12 na kutoa asisti 13 kwa Inter Miami inayoshika usukani wa Ligi Kuu Marekani maarufu MLS.
Messi kwa sasa anasubiri kuiwakilisha kwa mara nyingine Argentina katika fainali za Copa America zitakazofanyika nchini Marekani ambapo Argentina itakuwa ikiwania kulibeba taji hilo ambalo ililibeba mwaka 2021.
Akizungumzia maisha ya soka nchini Marekani, Messi alisema kwamba ulikuwa uamuzi mgumu kwa yeye kuondoka Ulaya na kuhamia Marekani lakini ushindi wake wa Kombe la Dunia umemfanya aweze kufikiria mambo kwa namna tofauti.
Messi pia alisema kwamba siku zote anapenda kucheza soka na kufanya mazoezi ya kujiandaa na mechi za kila mara lakini kidogo ana ameanza kuwa na hofu kwamba yote hayo yanaelekea mwisho hivyo analazimika kufurahia kila kitu kwa wakati huu.