Na mwandishi wetu
Hatimaye mwekezaji wa klabu ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ ameibuka na kueleza kukubali kuwa mwenyekiti mpya wa muda wa bodi ya wakurugenzi wa klabu hiyo na kujinasibu amerudi kwa ari na nguvu mpya.
Dewji ambaye amesisitiza kuwa sambamba na Simba katika nyakati zote ikiwemo hali wanayoipitia sasa, ameeleza hilo leo Jumatano baada ya jana Salim Abdallah ‘Try Again’ kutangaza kujiuzulu nafasi ya mwenyekiti wa bodi na kumuomba Dewji achukue nafasi hiyo.
“Ndugu zangu Wanasimba huu sio muda wa malumbano, kupakana matope, ni muda wa kusimama na kutengeneza timu yetu ili iwe bora zaidi ya ilivyokuwa awali.
”Ni wakati wa kupambana, kubuni mbinu, kuweka mikakati na kutekeleza hiyo mipango ya kuandaa Simba mpya, simba itakayotisha tena.
“Hivi karibuni nilikua na kikao na Mwenyekiti wa Bodi, Salim kupokea ripoti ya klabu yetu, nilimchagua ndugu Salim kuwa mwenyekiti wa bodi kwa kuwa nilishafanya naye kazi muda mrefu, namjua ni mtu mwaminifu na mtulivu.
”Namshukuru sana yeye na wajumbe wote wa bodi kwa kazi kubwa waliyofanya mpaka sasa, ameonesha nia ya kutaka kupumzika na kuniomba mimi nirudi kuwa mwenyekiti wa bodi,” alisema Dewji.
Dewji amefunguka kuwa amekubali kuwa mwenyekiti baada ya kushauriana na viongozi mbalimbali pamoja na bodi ya ushauri kwa kipindi hiki mpaka Simba itakaporejea kwenye hali yake ya kawaida.
“Wanasimba pia nimemuomba Salim kubaki kwenye bodi kwa niaba ya mwekezaji na amekubali na hivi punde nitateua wajumbe wengine kujaza nafasi ili bodi iwe kamili kuanza kufanya kazi,” alieleza Dewji na kuongeza:
“Narejea nikiwa na nguvu na ari mpya, maarifa ya kuirejesha Simba ninayo, naongozwa zaidi na ushabiki wa Simba na wala sio uwekezaji wala ufadhili, wala udhamini.
“Sitaiacha Simba leo wala kesho, niwaombe sana Wanasimba wenzangu mtulie, mtupe nafasi ya kujenga Simba mpya, Simba yenye matarajio na mabadiliko ili kila mwanasimba awe na furaha na atembee kifua mbele.
“Ningependa sana kuona Simba yenye utulivu na umoja ili tupate mafanikio makubwa, naomba tuache kelele, vijembe, hasira na makundi tuyazike yote kwa sasa, maana klabu yetu ipo kwenye kazi kubwa ya kusajili, kuna ‘pre-season’, Simba Day, Ngao ya Jamii na hatimaye ligi kuu, klabu ndiyo klabu kubwa Afrika kutoka Tanzania, tusisahau hilo,” alisema Dewji.
Hivi karibuni, Simba imekuwa kwenye msuguano uliopelekea baadhi ya viongozi wa juu kujiuzulu kutokana na matokeo yasiyoridhisha ya timu hiyo katika michuano wanayoshiriki.
Mafanikio ya wapinzani wao, Yanga SC kwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu NBC, Kombe la FA la CRDB pia kuwafunga nje ndani Simba, vimechangia ‘mvurugiko’ huo kwa Wekundu hao.