Warsaw, Poland
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Poland, Robert Lewandowski ataikosa mechi ya kwanza ya timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Ulaya (Euro 2024) dhidi ya Uholanzi baada ya kuumia misuli.
Lewandowski ambaye pia ni mshambuliaji wa Barcelona, aliumia juzi Jumatatu wakati wa mechi ya kirafiki dhidi ya Uturuki ambayo Poland ilitoka na ushindi wa mabao 2-1.
Poland itaumana na Uholanzi Jumapili ijayo, mechi ambayo itakuwa ya kwanza kwa timu hizo kwenye fainali za Euro 2024 zitakazoanza rasmi keshokutwa Ijumaa nchini Ujerumani.
Matarajio ya awali ni kwamba Lewandowski angecheza mechi na Uholanzi lakini aliumia dakika ya 33 katika mechi na Uturuki, mechi ambayo ni ya mwisho ya kujipima nguvu kwa timu hizo kabla ya kuanza rasmi kwa fainali za Euro 2024.
Baada ya mechi na Uholanzi, Poland itacheza mechi yake ya pili dhidi ya Austria hapo Juni 21 kabla ya kukamilisha mechi zake za Kundi D dhidi ya Ufaransa, mechi itakayopigwa Juni 25.
“Lewandowski amepata tatizo la misuli, ni tatizo ambalo litamfanya asiwemo kwenye mechi ya kwanza ya fainali hizi,” ilieleza taarifa ya Poland.
Wachezaji wengine wa Poland walioumia katika mechi hiyo ni beki Pawel Dawidowicz na mshambuliaji Karol Swiderski ambao baadaye ilielezwa kwamba watakuwa vizuri mapema.