Na mwandishi wetu
Meneja habari na mawasiliano Azam FC, Thabiti Zakaria amesema kuwa timu hiyo haitaweza kushiriki michuano ya Kombe la Kagame kutokana na kubanwa na ratiba ya michuano hiyo.
Akzungumza leo Jumatano jijini Dar es Salaam, Zakaria maarufu Zaka za Kazi amesema inakuwa ngumu kwa kuwa michuano hiyo itaanza Julai 6 na wao wanaanza maandalizi Julai 4, mwaka huu hivyo watakuwa wanakinzana.
“Michuano ya Kagame tunaitaka na tumebeba kombe mara mbili lakini inatuwia vigumu kushiriki kutokana na ratiba yenyewe ilivyo maana inaanza tarehe 6 na sisi tunarudi kuanza ‘pre-season’ tarehe 4.
“Sasa kwa afya ya soka haiko sawa maana yake hapo utawafosi wachezaji washindane wakiwa hawako tayari na inavyopaswa maandalizi kama ya mwanzo wa msimu yanachukua wiki sita, lakini vinginevyo itazalisha majeraha kwa wachezaji wengi kutokana na kukosa utayari,” alisema Zaka.
Alibainisha zaidi kuwa endapo kutarekebishwa ratiba ya michuano hiyo na angalau ikaanza Agosti, mwaka huu basi inaweza kuwa na afya nzuri kisoka na kupata ushindani unaotakiwa kutoka kwa kila timu.
Michuano hiyo inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) na kushirikisha timu 16, awali ilipangwa kuanza Julai 20 hadi Agosti 4 lakini kutokana na ratiba ya michuano ya klabu Afrika, imelazimika kubadilishwa tarehe na sasa itaunguruma kuanzia Julai 6 mpaka 22, mwaka huu.
Soka Azam yajitoa Kombe la Kagame
Azam yajitoa Kombe la Kagame
Read also