Amsterdam, Uholanzi
Timu ya taifa ya Uholanzi imepata pigo wakati ikijiandaa na fainali za Kombe la Ulaya (Euro 2024) baada ya kiungo wake Frenkie de Jong kuondolewa katika kikosi cha timu hiyo kutokana na kuwa majeruhi.
De Jong 27, amekuwa nje ya uwanja tangu aumie enka Aprili 21 mwaka huu katika mechi ya Barca na Real Madrid ambayo Barca ililala kwa mabao 3-2 ingawa ilitarajiwa angepona na kuwamo katika kikosi cha Uholanzi kwa ajili ya Euro 2024.
Kutokana na matumaini kwamba De Jong angepona, kocha wa Uholanzi, Ronald Koeman alimuita kiungo huyo katika kikosi chake cha wachezaji 26 lakini jana Jumatatu ilibainika kwamba hatoweza kuwa fiti.
De Jong alisema ilikuwa ndoto yake kuiwakilisha nchi yake katika mashindano hayo makubwa lakini kwa sasa kama ilivyo kwa taifa zima naye atakuwa akiishangilia timu hiyo akiwa nje ya uwanja.
“Nimesikitishwa na kukatishwa tamaa, sitokuwamo kwenye fainali za Euro, tumefanya juhudi kubwa katika wiki chache zilizopita lakini bahati mbaya tatizo la enka linalonisumbua linahitaji muda zaidi,” alisema De Jong.
Kiungo huyo ambaye ameichezea Uholanzi mara 54 alikosa mechi sita za mwisho za Barca baada ya kuumia na matarajio yaliyokuwapo ni kwamba muda ungetosha kumuwezesha kupona ili aiwakilishe Uholanzi kwenye fainali za Euro 2024.
Kwa upande wake Koeman aliulaumu uongozi wa Barca kwa namna ambavyo haujayapa uzito majeraha ya De Jong, matokeo yake timu ya taifa ya Uholanzi inajikuta ikimkosa mchezaji huyo.
Uholanzi itatupa karata yake ya kwanza kwenye fainali za Euro Juni 16 kwa kuumana na Poland na baada ya hapo itazikabili timu za Ufaransa na Austria kukamilisha mechi za hatua ya makundi.