Manchester, England
Klabu ya Manchester United imetangaza dau la Pauni 40 milioni kwa timu yoyote itakayomtaka winga wao, Jadon Sancho ambaye kwa sasa anaichezea kwa mkopo, Borussia Dortmund.
Sancho alilazimika kuuzwa kwa mkopo baada ya kuingia katika mzozo na kocha wake, Erik ten Hag aliyemtuhumu kwa kuzembea jambo ambalo mchezaji huyo alilipinga kwenye mitandao ya kijamii.
Akiwa Dortmund, Sancho, 24, ameiwezesha timu hiyo kufikia hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kukwama mbele ya Real Madrid walioibuka vinara kwa ushindi wa mabao 2-0.
Kutokana na mzozo ulioibuka baina ya Sancho na Ten Hag, hatma ya mchezaji huyo kurudi Man United imeendelea kuwa ndogo na ikitokea akarudi basi nafasi ya Ten Hag kubaki Man United nayo inazidi kuwa ndogo.
Kinachoonekana kwa sasa ni kwamba Man United imeamua kumuuza mchezaji huyo bila kujali nafasi ya Ten Hag ambaye ana mwaka mmoja katika mkataba wake na bado haijaamuliwa kama atabaki au ataondoka.
Kwa sasa Sancho amebakiza miaka miwili katika mkataba wake Man United na Dortmund wanataka kuendelea kuwa na winga huyo msimu ujao kwa mkopo wakati Man United wanataka kumpiga bei moja kwa moja.
Sancho alijiunga na Man United Julai 2021 kwa ada ya Pauni 73 milioni akitokea Dortmund, zipo habari kwamba anawindwa na klabu kadhaa Ulaya ikiwamo Man City ambayo aliwahi kucheza kwenye akademi yao miaka ya nyuma.
Kimataifa Sancho atupwa sokoni
Sancho atupwa sokoni
Read also