Rio de Janeiro, Brazil
Wanasoka wakongwe Brazil, Ronaldo de Lima na Rivaldo wamesema Vinícius Júnior tayari kafanya mambo ya kutosha kumpa tuzo ya Ballon d’Or baada ya kuiongoza Real Madrid kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Vinícius Jr au Vini alifunga bao Real Madrid ilipoilaza Borussia Dortmund mabao 2-0 Jumamosi iliyopita katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kubeba taji hilo ambalo linakuwa la 15 kwa klabu hiyo na la pili kwa Vini katika miaka yake sita na klabu hiyo.
Rivaldo ambaye alikuwa pamoja na Ronaldo katika kikosi cha Brazil kilichobeba Kombe la Dunia mwaka 2002 alisema Vinícius alihitaji kuboresha soka lake na kufunga mabao zaidi msimu huu ili abebe tuzo ya Ballon d’Or.
Baada ya Vinícius kuifungia Real Madrid mabao 24 katika mashindano yote msimu huu, Rivaldo amesema kwamba anaamini mchezaji huyo amefanya jambo linalotosha kumpa tuzo hiyo.
“Ni kijana anayejituma, aliwasili Real Madrid na kwenda timu B kujifunza, alicheza mechi chache na tuliweza kuona kwamba alihitaji muda zaidi wa kujifunza kufunga mabao.

“Na alichofanya ni kujifunza, alifanya mazoezi kwa bidii, alijitoa, na leo unaweza kuona amekuwa na urahisi katika kufunga,” alisema Rivaldo.
Kwa upande wa Ronaldo, alisema kwamba anadhani Vini ana sifa zote za kuchukua Ballon d’Or baada ya kuwa na msimu mzuri katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na La Liga.
“Nafikiri wakati wake umefika, amekuwa vizuri mno kwa mwaka huu, na leo ndiye mchezaji bora duniani tena kwa mbali,” alisema Ronaldo.