Na mwandishi wetu
Wadhamini wa klabu ya Yanga, Kampuni ya SportPesa imewakabidhi viongozi wa timu hiyo hundi ya Sh milioni 537.5 ikiwa ni ‘bonus’ ya kufanya vizuri kwa timu hiyo msimu huu.
Zoezi hilo limefanyika leo Jumatano jijini Dar es Salaam ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa SportPesa, Abbas Tarimba amewapongeza viongozi na wafadhili wa Yanga, GSM kuwa ni watu wenye njaa ya mafanikio ndio maana Yanga imekuwa kubwa Afrika sasa.
“Young Africans SC imekuwa ikiendeshwa kiuweledi. Hii inatokana na kuwa na viongozi wenye njaa ya mafanikio. Nguvu hiyo imeifanya kuingia kwenye moja ya klabu bora tatu barani Afrika.
“Nimpongeze sana Rais wa Yanga, Hersi Said kwa jitihada zake kwa klabu hii. Sisi kama Kampuni ya SportPesa vile vile tunampongeza mdhamini na mfadhili wa Young Africans SC, Ghalib Said Mohamed (GSM) kwa mchango wake mkubwa kwa klabu hii. Bila shaka amefanya kazi kubwa, tunapenda salamu zetu zimfikie,” alisema Tarimba.
Pia, Tarimba ambaye ni mdau wa Yanga, aliwapongeza wachezaji wa timu hiyo kwa namna walivyopambana na kutokata tamaa hata walipokosa penalti za awali kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho CRDB dhidi ya Azam FC, mechi iliyopigwa Zanzibar kabla ya baadaye kufanikiwa kunyakua kombe hilo kwa mikwaju ya penalti 6-5.
Naye Rais wa Yanga, Hersi Said aliwashukuru SportPesa kwa kuwa nao bega kwa bega huku akiwaahidi kuwa Yanga itaendelea kupambana zaidi kufikia ndoto zake Afrika wakiwa sambamba na kampuni hiyo.
Yanga ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu NBC na Kombe la Shirikisho CRDB, wamepewa kiasi hicho cha fedha kutokana na kupambana kwao kufika hatua ya robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa mujibu wa mkataba, Yanga hupewa bonus na SportPesa kwa kila hatua wanayofika kwenye michuano hiyo ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf).