Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa, Kylian Mbappe amesema kuna mambo na baadhi ya watu waliomfanya asifurahie maisha katika msimu wake wa mwisho akiwa na klabu ya PSG.
Mbappe, 25, kwa sasa anasubiri kujiunga na kutambulishwa rasmi na katika klabu ya Real Madrid ya Hispania mara baada ya mkataba wake wa sasa na PSG utakapofikia ukomo Juni 30 mwaka huu.
Hatua ya Mbappe kwenda Real Madrid imekuja baada ya uvumi wa muda mrefu ukimhusisha na klabu hiyo wakati huo huo vigogo PSG nao wakijaribu kumshawishi asaini mkataba mwingine na klabu hiyo ya jijini Paris.
“Pale PSG sikuwa mtu niliyekosa raha, kusema nilikosa raha itakuwa kama kung’ata mkono unaokupa kula na kuwatemea mate watu wote walionitetea lakini kuna mambo na watu walionifanya nikose raha,” alisema Mbappe.
Mbappe hata hivyo pamoja na kukiri hilo lakini alisema kuna baadhi ya mambo ambayo hangeweza kuyaonesha kwa sababu alikuwa kiongozi na hivyo asingeweza kuungana na mtu ambaye anataka kubeba ajenda za huzuni.
Akimzungumzia kocha wake wa PSG, Luis Enrique alisema kocha huyo pamoja na mshauri Luis Campos walimuokoa na bila wao asingeweza kamwe kucheza soka.
Mbappe pia alijivunia msimu uliomalizika hivi karibuni wa 2023-24 hasa baada ya kujua mambo aliyotakiwa kuyapitia ili aweze kucheza soka.
“Kwa viwango vyangu ni msimu ambao nilikuwa chini lakini nilicheza mechi mara kwa mara na kushinda makombe, hilo ni jambo kubwa ninalojivunia lakini mwakani siwezi kuridhishwa kwa msimu kama huu,” alisema Mbappe.
Mbappe ameiwezesha PSG kushinda mataji ya Ligi 1 mara sita na kwa sasa anaangalia changamoto mpya kuanzia msimu ujao wa 2024-25 atakapoanza kuichezea Real Madrid, timu ambayo ndio kwanza imetoka kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.