Napoli, Italia
Kocha wa zamani wa timu za Chelsea na Tottenham Hotspur, Antonio Conte ameteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya Napoli ya Italia kwa mkataba wa miaka mitatu.
Conte, 54, amekabidhiwa jukumu hilo ikiwa ni takriban mwaka mmoja na miezi miwili sasa tangu aachane na Spurs baada ya kuwa na timu hiyo kwa mwaka mmoja na miezi minne.
Akiwa na Chelsea, Conte alifanikiwa kuiwezesha timu hiyo kubeba taji la Ligi Kuu England (EPL) katika msimu wa 2016-17 pamoja na lile la FA kabla ya kutimuliwa mwaka 2018.
“Napoli ni sehemu yenye umuhimu wake duniani, nina furaha na naona ufahari katika jambo hili, kukaa katika benchi la bluu,” alisema Conte ambaye pia aliwahi kuinoa Inter Milan na mwaka 2021 aliiwezesha timu hiyo kubeba taji la kwanza la Serie A baada ya miaka 11.
“Naweza kuahidi jambo moja, nitafanya kila ninaloweza kwa maendeleo ya timu na klabu hii, kujituma kwangu pamoja na maofisa wengine kutakuwa ni kwa mapana,” alisema Conte.
Conte ambaye ni Mtaliano si jina geni katika soka la Italia kwamba mbali na Inter Milan pia aliwahi kuinoa Juventus na kuiwezesha kubeba mataji matatu ya Serie A kati ya mwaka 2011 na 2014.
Napoli ambayo msimu uliopita ilibeba taji la Serie A ikiwa ni mara ya kwanza baada ya miaka 33, msimu huu imeshindwa kuonesha ubora wake na imemaliza ligi ya Serie A ikiwa nafasi ya 10.
Mwenendo mbaya wa timu hiyo msimu huu ulisababisha kutimuliwa kwa kocha Francesco Calzona ambaye alipewa jukumu hilo Februari mwaka huu akiwa kocha wa muda baada ya kutimuliwa kwa Walter Mazzarri.