Madrid, Hispania
Mshambuliaji Kylian Mbappe hatimaye amesaini mkataba kujiunga na klabu ya Real Madrid akiwa huru mara mkataba wake wa sasa na PSG utakapofikia ukomo Juni 30 mwaka huu.
Mbappe ambaye amekuwa akihusishwa na timu hiyo katika siku za karibuni, Februari mwaka huu alikubali kwa maneno kuwa atajiunga na timu hiyo na mwezi uliopita alitangaza kuwa anaondoka PSG baada ya msimu huu.
Habari zaidi zinadai kwamba tayari mshambuliaji huyo ameshasaini na Real Madrid na atajiunga na timu hiyo ya Hispania mara msimu mpya wa La Liga wa 2024-25 utakapofunguliwa rasmi hapo Julai Mosi mwaka huu.
Kwa upande wa Real Madrid wanatarajia kumtangaza mshambuliaji huyo mapema wiki ijayo na huenda wakamtambulisha rasmi kwenye dimba la Bernabeu kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Ulaya 2024 au Euro 2024 zitakazofanyika hivi karibuni nchini Ujerumani.
Mbappe, 25 amekuwa mmoja wa washambuliaji mahiri duniani tangu ajiunge na PSG mwaka 2017 akitokea Monaco, ndiye mshambuliaji mwenye rekodi ya mabao mengi PSG (mabao 256), mwaka 2018 aliiwezesha Ufaransa kubeba Kombe la Dunia.
Katika makubaliano na Real Madrid, Mbappe amekubali kusaini mkataba utakaofikia ukomo mwaka 2029 akilipwa Pauni 12.8 milioni kwa kila msimu pamoja na marupurupu mengine na atakuwa na sehemu ya mgawo katika malipo ya matangazo atakayotumika.
Kimataifa Mbappe asaini Real Madrid
Mbappe asaini Real Madrid
Read also