Na mwandishi wetu, Zanzibar
Baada ya dakika 120 za mpambano wa kukata na shoka hatimaye Yanga imeibuka kinara wa Kombe la Shirikisho CRDB ikiilaza Azam FC kwa penalti 6-5 baada ya kila timu kupiga penalti mara tisa.
Katika mechi hiyo iliyopigwa leo Jumapili usiku kwenye dimba la New Amaan Complex, timu hizo zilioneshana ubabe kwa dakika 90 za kawaida bila kufungana na katika dakika 30 za nyongeza pia hakuna timu iliyoliona lango la mwenzake.
Baada ya dakika 120 kukamilika ndipo mwamuzi Ahmed Arajiga kutoka Arusha alipoamuru timu hizo ziiingie katika mikwaju ya penalti.
Walikuwa ni Yanga walioanza kupiga penalti kupitia kwa Stephane Aziz Ki ambaye alikosa kama ilivyokuwa kwa Joseph Guede na Ibrahim Bacca.
Waliofunga penalti za Yanga na kuipa timu hiyo kombe hilo ni Pacome Zouazoua, Yao Kouasi, Bakari Mwamnyeto, Khalid Aucho, Kennedy Musonda na Jonas Mkude.
Kwa upande wa Azam, penalti zao zilifungwa na Adolf Mtasingwa, Sidibe, Kipre Jr, Edward Manyama na Fei Toto ambaye baada ya kuujaza mpira wavuni aliwageukia mashabiki na kuwaonesha ishara ya kuwataka wakae kimya.
Waliokosa penalti za Azam ni Mendoza, Djibril Silla, Lusajo Mwaikenda na Idd Nado aliyekuwa wa mwisho kupiga penalti ambaye kukosa kwake ndiko kulikoamsha shwange za wachezaji na mashabiki wa Yanga.
Katika dakika 90 za kawaida pamoja na 30 za nyongeza, kila timu ilionesha uwezo wa kufanya mashambulizi na kama kuna mchezaji ambaye ameibuka shujaa katika muda huo basi ni kipa wa Azam, Mohamed Mustapha.
Mustapha aliokoa michomo iliyoelekezwa langoni mwake mara kadhaa lakini anaweza kukumbukwa zaidi kwa kuwanyima mabao Clement Mzize, Aziz Ki, Mudathir Yahya na Lomalisa ambao mashuti yao ama yaliishia mikononi mwake au kuokoa mpira na kuwa kona.
Soka Yanga yatwaa taji Shirikisho CRDB
Yanga yatwaa taji Shirikisho CRDB
Read also