London, England
Real Madrid usiku wa kuamkia leo Jumapili wameweka rekodi ya kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya 15 huku kocha wao, Carlo Ancelotti akijiwekea rekodi ya kubeba taji hilo mara tano.
Mabao mawili ya Dani Carvajal na Vinicius Jr ndiyo yaliyoiwezesha Real Madrid kuibwaga Borussia Dortmund katika mechi hiyo ya fainali iliyopigwa kwenye dimba la Wembley.
Real Madrid imeonesha uwezo wa kubadili matokeo kama ilivyokuwa katika fainali dhidi ya Liverpool mwaka 2022 na dhidi ya mahasimu wao wa jiji la Madrid, Atletico Madrid mwaka 2014, timu ambazo zilijipa matumaini makubwa ya kufuta ubabe wa Real Madrid.
Ikiwa na kipa wake mkongwe aliyekuwa majeruhi, Thibaut Courtois, Real Madrid ilipata upinzani kwa Dortmund waliotengeneza nafasi kadhaa ambazo hata hivyo hazikuweza kuzaa matunda.
Karim Adeyemi alipata nafasi nzuri lakini alishindwa kuchukua maamuzi ya haraka kuipatia timu yake bao kama ilivyokuwa kwa Niclas Fullkrug ambaye shuti lake liligonga mwamba na kurudi uwanjani.
Mashambulizi hayo yaliwapa matumaini Dortmund kwamba wangeweza kuuangusha mfupa uliowashinda vigogo wengine wa Ulaya lakini walianza kuangamizwa na Carvajal dakika ya 74 aliyeitumia vizuri pasi ya Toni Kroos kuandika bao la kwanza kwa kichwa.
Dakika takriban 10 baadaye, Vinicius alikamilisha hesabu kwa bao la pili na kuwahakikishia mashabiki wa Real Madrid kwamba huu tena ni mwaka wao akiitumia vizuri pasi ya Jude Bellingham.
Moto waliouonesha Real Madrid umedhihirisha kwamba timu hiyo hadhi yake ni taji hilo kubwa la klabu lenye hadhi na utajiri barani Ulaya kama si duniani kwa ujumla.
Kwa hali ilivyo, je ipo timu yeenye uwezo wa kuizuia Real Madrid kubeba taji hilo kwa mara ya 16 katika msimu ujao wa 2024-25 wakati ambao timu hiyo inajiandaa kumchukua Kylian Mbappe, mshambuliaji tishio duniani.
Kimataifa Real Madrid wabeba ndoo Ulaya
Real Madrid wabeba ndoo Ulaya
Read also