Munich, Ujerumani
Sasa ni rasmi, Bayern Munich hatimaye imemtangaza rasmi Vincent Kompany kuwa kocha mkuu mpya baada ya makubaliano na klabu ya Burnley ambayo kocha huyo alikuwa na mkataba nayo.
Inadaiwa Kompany amesaini mkataba wa miaka miwili na Bayern imelazimika kuilipa Burnley Pauni 10 milioni na sasa ni rasmi Kompany anakuwa kocha mpya akichukua nafasi iliyoachwa na Thomas Tuchel.
Kompany alijipatia umaarufu baada ya kuiwezesha Burnley kupanda daraja na kucheza Ligi Kuu England (EPL) ingawa katika msimu huo huo wa kwanza EPL timu hiyo imeshuka daraja na msimu ujao wa 2024-25 itacheza ligi ya Championship.
Uteuzi wa Kompany umekuja baada ya mabosi Bayern kupitia wakati mgumu kumsaka mrithi wa Tuchel ambaye, Februari mwaka huu klabu hiyo ilitangaza kuachana naye baada ya msimu huu.
“Ninajiandaa kwa changamoto ya FC Bayern, ni heshima kubwa kuweza kufanya kazi katika klabu hii, FC Bayern ni taasisi katika soka la kimataifa,” alisema Kompany.
Naye mkurugenzi wa michezo wa Bayern, Max Eberl alisema klabu yake ina furaha kubwa kumpata Kompany na wamefikia makubaliano haraka baada ya mazungumzo na kocha huyo kuonesha ni kwa kiasi gani amevutiwa na kazi ya kuinoa Bayern.
“Vincent Kampany ana njaa ya mafanikio na anawezesha kila kitu kufanikishwa, akiwa mchezaji tayari alionesha hulka za kiuongozi katika soka la kimataifa na anaendelea na hilo akiwa kocha,” alisema Eberl.
Kabla ya kumpata Kompany, Bayern walihusishwa na mipango ya kumchukua kocha wa Bayer Leverkusen, Xabi Alonso na kocha wao wa zamani ambaye kwa sasa anainoa timu ya taifa ya Ujerumani, Julian Nagelsmann, lakini wote walikataa.
Mwingine aliyetajwa kuwindwa na Bayern ni kocha wa zamani wa muda wa Man United, Ralf Rangnick ambaye pia aliamua kuendelea na kibarua chake cha kuinoa timu ya taifa ya Austria, hapo hapo kukawa na habari kwamba wangeendelea na Tuchel lakini pia haikuwezekana.