Na mwandishi wetu
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), Almasi Kasongo ameeleza kufurahishwa na namna ushindani ulivyoshamiri kwa mchezaji mmoja mmoja msimu huu kwenye Ligi Kuu NBC.
Amesema ukiachilia mbali kila timu kujitafuta katika malengo yake ya msimu na kuleta presha lakini pia ushindani wa mchezaji mmoja mmoja umekuwa tija kubwa katika kuchagiza ubora wa ligi ya msimu huu iliyofungwa rasmi jana Jumanne.
Akitoa mfano, Kasongo alisifia namna alivyokoshwa na ushindani wa Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC aliyemaliza na mabao 19 na Stephane Aziz Ki wa Yanga aliyeibuka kinara kwa mabao 21.
Kasongo pia alizungumzia ushindani wa kipa wa Coastal Union, Lqy Matampi aliyemaliza na ‘clean sheets’ 15 dhidi ya Djigui Diarra wa Yanga mwenye 14.
“Ushindani uliojitokeza ni faida kwa mpira wa miguu kiujumla, ni ushindani mzuri, kama Fei na Aziz huku Matampi na Diarra, kwetu sisi ni kitu kizuri kwa hiyo unaweza kuona kumbe unapokuwa mwisho wa mwaka wa soka kuna zoezi la kutambua mchezaji mmoja mmoja na mnakuja kugundua kwamba ni kitu ambacho kinaongeza thamani kwenye ligi kwa ujumla.
“Maana unaona kwamba kila mchezaji anapambana ili aweze kupata zawadi ya mchezaji mmoja mmoja na mchezaji anapopambana inakuwa faida kwa timu yake na kitendo cha kutambua mchango wa mchezaji mmoja mmoja inakuwa fursa, faida kwa timu na faida kwa mashabiki wanaofuatilia,” alisema Kasongo.
Ushindani wa Fei na Aziz Ki ulikwenda mpaka siku ya mwisho ambapo kila mmoja aliingia uwanjani akiwa na mabao 18 kama ilivyokuwa kwa Matampi na Diarra ambao wote waliingia dimbani wakiwa na clean sheets 14.
Mwisho wa siku matokeo ya ushindi wa 4-1 walioupata Yanga dhidi ya Tanzania Prisons na matokeo ya suluhu baina ya Coastal na KMC yalitoa majibu ya vinyang’anyiro hivyo.