Madrid, Hispania
Kiungo wa Real Madrid na timu ya taifa ya England, Jude Bellingham ameshinda tuzo ya mwanasoka bora wa msimu wa La Liga akiwa katika mwaka wake wa kwanza nchini Hispania.
Bellingham, 20, alijiunga na Real Madrid mwanzoni mwa msimu huu akitokea, Borussia Dortmund, hadi sasa ameifungia timu hiyo mabao 19 na kuiwezesha kubeba taji la La Liga kwa kuwaacha mahasimu wao Barcelona walioshika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi 10.
Nyota huyo mzaliwa wa Stourbridge pia katika Ligi ya Mabingwa Ulaya ameifungia timu hiyo mabao manne na keshokutwa Jumamosi, timu hiyo itaumana na Dortmund katika mechi ya fainali ya ligi hiyo kwenye dimba la Wembley.
Katika kinyang’anyiro cha kusaka tuzo hiyo, Bellingham aliwashinda mchezaji wenzake wa Real Madrid, Vinicius Jr, Antoine Griezmann wa Atletico Madrid, Artem Dovbyk wa Girona na Robert Lewandowski wa Barcelona.
Mshindi wa tuzo hiyo hupatikana kwa kupigiwa kura na mashabiki, manahodha wa timu pamoja na jopo la wataalam na kwa Bellingham, akiwa Dortmund pia alitwaa tuzo ya mwanasoka bora wa msimu wa 2022-23.
“Ningependa kuitoa tuzo hii kwa wachezaji wenzangu, makocha na zaidi ya yote mashabiki wa klabu hii bora duniani,” alisema Bellingham.
Bellingham hata hivyo hakuweza kuhudhuria hafla ya utoaji tuzo hiyo iliyofanyika Jumanne jioni kwa kuwa anajiandaa kwa mechi ya Jumamosi dhidi ya Dortmund.