Barcelona, Hispania
Kocha mpya mtarajiwa wa Barca, Hansi Flick amewasili jijini Barcelona ili kusaini mkataba na kukabidhiwa rasmi majukumu ya kuinoa timu hiyo baada ya kutimuliwa kwa Xavi Hernandez.
Flick, 59, amekuwa bila kazi tangu Septemba mwaka jana alipotimuliwa timu ya taifa ya Ujerumani na katika siku za hivi karibuni amekuwa akihusishwa na Barca ili kumrithi Xavi.
Kocha huyo aliwasili Barcelona Jumanne akiwa na wakala wake Pini Zahavi ili kukamilisha taratibu za kimkataba kabla ya kuanza majukumu hayo mapya huku zikiwapo habari kuwa atasani mkataba wa miaka miwili.
Flick ambaye pia amewahi kuinoa Bayern Munich, habari za kujiunga kwake na Barca zilianza kusikika Januari mwaka huu baada ya Xavi kutangaza kwamba ataachana na timu hiyo baada ya msimu huu.
Aprili mwaka huu mambo yalibadilika baada ya Xavi kubadili uamuazi wa awli na kuamua kuwa angeendelea kuinoa timu hiyo hadi mkataba wake utakapofikia ukomo mwaka 2025.
Mambo hata hivyo yalibadilika kwa mara nyingine baada ya Rais wa Barca, Joan Laporta kuamua kumtimua Xavi sababu ikidaiwa kuwa ni kauli ya kocha huyo kwamba timu hiyo haitoweza kushindana na timu kubwa Ulaya kwa sababu ya matatizo ya kiuchumi.
Baada ya hapo, Laporta alimgeukia Flick ambaye inadaiwa alikuwa akimpigia hesabu tangu mwaka 2021 ili achukue nafasi ya Ronald Koeman lakini Flick ambaye wakati huo alikuwa akiinoa Bayern tayari alikuwa na makubaliano na timu ya taifa ya Ujerumani.
Moja ya mafanikio ya kukumbukwa ya Flick ni yale ya mwaka 2020 akiwa Bayern alipoiwezesha timu hiyo kubeba mataji matatu makubwa, mawili ya Ujerumani pamoja na lile la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kimataifa Hansi Flick awasili Barcelona
Hansi Flick awasili Barcelona
Read also