Na mwandishi wetu
Baada ya kushindwa kunyakua kiatu cha ufungaji bora, kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amempongeza kinara wa mabao Stephane Aziz Ki wa Yanga japo na yeye anafurahia timu yao kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika.
Fei Toto aliyemaliza Ligi Kuu NBC akiwa na mabao 19, amempongeza kiungo wa Yanga Aziz Ki aliyefunga mabao 21 ambapo Fei pia amekiri kuwa mchezaji huyo alistahili kwa namna ambavyo alipambana.
“Hata kama nimekosa kiatu lakini najisikia vizuri tu, unajua jambo la kwanza ni timu na mengine baadaye. Kwa hiyo nampongeza sana (Aziz Ki) kwa kuwa mfungaji bora na pia tuna furaha tumefuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kama timu.
“Maana jambo la kwanza lilikuwa kufuzu na mengine baadaye, tuangalie hayo baadaye,” alisema Fei aliyejiunga na Azam msimu huu akitokea Yanga.
Fei ambaye pia ametoa pasi za mabao saba, akizidiwa mbili na Kipre Junior (Azam) mwenye tisa ameeleza kuwa anaamini huu ndio msimu wake bora zaidi tangu aanze kucheza Ligi Kuu NBC alipotua Yanga msimu wa 2018-19.
“Niseme kweli, ni wazi huu ndio msimu wangu bora tangu nianze kucheza Ligi ya Tanzania Bara kwa hiyo namshukuru Mungu kwa kumaliza msimu salama salmini bila ya majeraha na najiskia furaha,” alisema Fei.
Fei aliongeza kwamba kwake yeye hiyo ni historia kubwa na la muhimu zaidi ni kujitunza, kufanya mazoezi kwa bidii, kumsikiliza kocha na mambo mengine yataaenda vizuri.