Barcelona, Hispania
Kocha aliyetimuliwa Barcelona, Xavi Hernandez amesema kwamba kocha mpya atakayebeba majukumu yake katika timu hiyo atapata tabu.
Xavi, 44, alitangazwa kutimuliwa rasmi na timu hiyo kabla ya kuiongoza katika mechi ya mwisho ya kumaliza msimu dhidi ya Sevilla juzi Jumamosi, mechi ambayo Barca ilipata ushindi wa mabao 2-1.
Mara baada ya Xavi kutimuliwa habari zilizopo ni kwamba kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani na klabu ya Bayern Munich, Hansi Flick anatazamiwa kubeba majukumu yake.
Xavi, ambaye alikuwa na mkataba Barca unaofikia ukomo mwaka 2025, Januari mwaka huu alitangaza angeondoka mara baada ya msimu huu lakini alibadili msimamo mwezi uliopita akidai kwamba anatarajia kuendelea na mkataba wake.
Akimzungumzia kocha mpya wa Barca, Xavi alisema kwamba atapata tabu kwa sababu klabu hiyo ni sehemu iliyojaa utata na ni kazi ngumu.
“Nakwambia ‘utapata tabu’, hii ni sehemu yenye utata na ni kazi ngumu na unalazimika kuwa mtulivu,” alisema Xavi.
Xavi aliyekabidhiwa jukumu la ukocha Barca, Novemba 2021, katika msimu wake wa kwanza kamili alibeba taji la La Liga na Spanish Super lakini msimu huu mambo hayajawa mazuri, timu hiyo imemaliza ligi nafasi ya pili nyuma ya mahasimu wao Real Madrid kwa tofauti ya pointi 10.
“Ninachokiona ni kwamba kila nilichokifanya kwa miaka miwili na nusu kimezua mabalaa, nimekuwa nikiwindwa mara nyingi na katika mazingita mengi,” alisema Xavi.