Na mwandishi wetu
Kuelekea mechi ya kufunga msimu wa 2023-24, kaimu kocha mkuu Simba, Juma Mgunda amesema wanahitaji kufunga hesabu zao vizuri kwa kuhakikisha wanaibuka na ushindi dhidi ya JKT Tanzania kesho Jumanne.
Akizungumza leo Jumatatu kocha huyo wa zamani wa Coastal Union alisema mechi yao hiyo itakayochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam itakuwa na ushindani mkubwa kwani wanafahamu JKT pia wanauhitaji ushindi wa kesho ili kusalia Ligi Kuu NBC.
“Mechi ya kesho ni ya maamuzi, na mechi yoyote yenye kuhitaji maamuzi inategemea ni mahitaji gani yanahitajika, kila mmoja ana mahitaji yake, Simba tuna mahitaji yetu ya mchezo huo na JKT pia wana mahitaji yao, kwa hiyo naamini itakua mechi yenye ushindani na mwisho lazima itoe maamuzi.
“Sababu kesho kama nilivyosema ndio kama tunafunga shule, unapofuga shule lazima ujue mtihani wako umekuwaje, matokeo yako kiujumla yakoje, lakini kubwa nataka niseme tunajua umuhimu wa mechi ya kesho, tumejiandaa kuhakikisha licha ya kufanya vizuri lakini pia tunapata matokeo mazuri,” alisema Mgunda.
Naye kocha msaidizi wa JKT, George Mketo alisema: “Tumejiandaa na mchezo wa simba hapo kesho, tunaamini hauwezi kuwa mchezo rahisi, utakuwa mgumu kulingana na mahitaji ya timu zote mbili, sisi tunahitaji kupata alama kwa ajili ya kubaki ligi kuu lakini Simba wanahitaji ushindi ili wamalize wa pili.
“Lakini tumeitazama Simba kwa timu yao, ubora wao na tunaamini ni timu kubwa na ina uzuri wa wachezaji waliokomaa kwa hiyo nasi kulingana na ugumu wa mchezo tutawaheshimu kulingana na mahitaji tunayoyahitaji kwa kuhakikisha tunapata alama tukiwa na mpango wetu kuhusiana na hilo.”
JKT inashika nafasi ya 12 kwa pointi 32, pointi moja zaidi ya Kagera Sugar inayoshika nafasi ya 13. JKT inahitaji ushindi ili kukimbia kushuka chini na kuwa miongoni mwa timu nne zitakazoanza mchakato wa kujinasua kutoshuka daraja.