Na mwandishi wetu
Yanga leo Jumamosi imekabidhiwa taji la Ligi Kuu NBC msimu wa 2023-24 huku ikiziacha Simba na Azam FC zikichuana vikali kuwania nafasi ya pili wakati huo huo viungo washambuliaji, Fei Toto na Aziz Ki kila mmoja akikitolea macho kiatu cha mfungaji bora.
Yanga imekabidhiwa taji hilo ambalo sasa wanakuwa wamelibeba mara ya nne mfululizo baada ya kuinyuka Tabora United mabao 3-0, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam.
Baada ya matokeo hayo, mashabiki, viongozi, wachezaji baadhi wakiwa na familia na jamaa zao wa karibu walilipuka kwa shangwe kufurahia ubingwa huo.
Ukiachana na furaha ya Yanga, mbio za kusaka nafasi ya pili zinazidi kupamba moto kwa Simba na Azam baada ya timu hizo zote kunyakua pointi tatu muhimu katika mechi zao za leo.
Kazi iliyobaki sasa ni kwa kila timu kuhakikisha inapata ushindi katika mechi moja iliyobaki ingawa Azam kwa sasa ndiyo iliyo mbele ya Simba.
Simba imeinyuka KMC bao 1-0 na hivyo kufikisha pointi 66 sawa na Azam ambayo imeibugiza Kagera Sugar mabao 5-1 na hivyo kuwa pointi sawa na Simba lakini Azam inajivunia wastani mzuri wa mabao na hivyo kuendelea kushika nafasi ya pili Simba ikibaki ya tatu.
Azam imefikisha mabao 61 wakati Simba ina mabao 57, Azam imefungwa mabao 21 wakati Simba imefungwa mabao 25, timu zote hizo kila moja imetoka sare mara sita na kupoteza mara tatu na kila moja imecheza mechi 29 na imebakiwa na mchezo mmoja.
Aziz Ki, Fei Toto usipime
Nje ya vita ya Simba na Azam kuisaka nafasi ya pili, ipo vita nyingine ya viungo washambuliaji, Feisal Salum au Fei Toto wa Azam dhidi ya Stephanie Aziz Ki wa Yanga, wachezaji ambao wamewahi kucheza pamoja katika kikosi cha Yanga kabla ya Fei Toto kutimkia Azam.
Mabao mawili aliyofunga Fei Toto leo dhidi ya Kagera Sugar yamemfanya amfikie Aziz Ki kwa kufikisha mabao 18 ambayo pia anayo Aziz Ki kwani naye amefunga bao leo katika ushindi wa Yanga wa 3-0 dhidi ya Tabora.
Kama ilivyo kwa Simba na Azam, Fei Toto na Aziz Ki nao kila mmoja anasubiri mechi ya mwisho ya kufunga msimu huu wa Ligi Kuu NBC ili kujua kama ataibuka kinara wa mabao au la.
Matokeo ya mechi za Ligi Kuu NBC leo Jumamosi…
Yanga 3-0 Tabora United
Kagera Sugar 1-5 Azam
Simba 1-0 KMC
Coastal Union 0-0 JKT Tanzania
Ihefu FC 0-2 Dom Jiji
Mashujaa 3-2 Mtibwa Sugar
Namungo 2-2 Prisons
Singida 2-1 Geita Gold
Soka Yanga yakabidhiwa taji, nafasi ya 2 moto
Yanga yakabidhiwa taji, nafasi ya 2 moto
Read also