Munich, Ujerumani
Klabu za Bayern Munich ya Ujerumani na Burnley ya England inadaiwa zipo katika hatua za mwisho kufikia makubaliano ili kocha wa Burnley, Vincent Kompany asaini mkataba wa kuinoa Bayern Munich.
Bayern, hivi karibuni iliachana na kocha Thomas Tuchel, hatimaye inadaiwa kumgeukia Kompany ambaye amewahi kuwa na klabu ya Hamburg pia ya Ujerumani kwa miaka miwili lakini pia ana uwezo wa kuzungumzia vizuri Kijerumani.
Hatua ya kumgeukia Kompany ambaye timu yake ya Burnley imeshuka daraja, imekuja baada ya makocha Xabi Alonso, Julian Nagelsmann na Ralf Rangnick kukataa ofa ya kuinoa timu hiyo na sasa akili imeelekezwa kwa Kompany.
Habari za ndani zinadai kwamba Bayern wanaamini kuwa Kompany, beki wa zamani wa Man City na timu ya taifa ya Ubelgiji, yuko tayari kwa kazi hiyo kama makubaliano yatafikiwa na Burnley.
Katika mpango huo, Bayern watapenda kuona Kompany anajiunga na timu hiyo ya mjini Munich pamoja na wasaidizi wake akiwamo mshambuliaji wa zamani wa Wales, Craig Bellamy.
Kompany alijiunga na Burnley mwaka 2022 akitokea Anderlecht ya Ubelgiji, katika msimu wake wa kwanza aliiwezesha Burnley kubeba taji la Championship ikikusanya pointi 101 na kufuzu kucheza Ligi Kuu England (EPL).
Timu hiyo hata hivyo katika msimu wa kwanza EPL imeshika nafasi ya 19 na kushuka daraja, hivyo msimu ujao wa 2024-25 itarudi katika Ligi ya Championship.
Kwa Kompany jina lake limeendelea kuwa juu licha ya Burnley kushuka, Pep Guardiola inadaiwa aliwahi kumtaja akimhusisha na kazi ya ukocha Man City, timu aliyoichezea kwa mafanikio kwa miaka 11, majira ya kiangazi msimu uliopita pia alihusishwa na timu za Tottenham na Chelsea.
Kimataifa Stori ya Kompany, Bayern yapamba moto
Stori ya Kompany, Bayern yapamba moto
Read also