Manchester, England
Siku moja kabla ya Man United na Man City kuumana katika fainali ya Kombe la FA, kocha wa Man City, Pep Guardiola ameanza kuijadili hatma ya mwenzake wa Man United, Erik ten Hag akidai kwamba akishindwa mechi hiyo atakuwa matatizoni.
Man City na Man United zinaumana huku Man City ikiwa imetoka kubeba taji la Ligi Kuu England (EPL) na sasa inasaka taji la pili wakati Man United inapitia msimu mgumu na inasaka taji hilo ili walau ishiriki michuano ya Europa Ligi.
Pep alionekana kumsikitikia Ten Hag kutokana na majanga ya wachezaji majeruhi yanayomkabili lakini hapo akasema makocha wa klabu kama Man United wanaopitia katika msimu mgumu wakati wote wanakuwa katika wakati mgumu.
“Kwa klabu kubwa kama United au City, inapokuwa hushindi mechi zako wakati wote unakuwa katika matatizo,” alisema Pep.
“Hata mimi ningekuwa matatizoni kama nisingekuwa nashinda, Ten Hag amefanya mengi mazuri, ninamheshimu sana kwa kazi yake ya siku za nyuma na hata sasa akiwa na United,” aliongeza Pep.
Habari za ndani Man United zinadai kuwa Ten Hag huenda akatimuliwa mara baada ya mechi hiyo na City itakayopigwa kwenye dimba la Wembley na tayari makocha kadhaa wamekuwa wakitajwa kuchukua nafasi yake.
Makocha hao ni Mauricio Pochettino aliyeachana na Chelsea katika siku za karibuni, Thomas Frank, Kieran McKenna na Thomas Tuchel aliyekuwa akiinoa Bayern Munich.