Barcelona, Hispania
Mshambuliaji wa Barcelona, Robert Lewandowski amesema kwamba timu yao haina hofu yoyote juu ya ujio wa Kylian Mbappe anayejiunga na mahasimu wao, Real Madrid.
Msimu huu Real Madrid imekuwa tishio katika Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’, ndiyo inayoshika usukani ikiizidi Barca inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi 12 na wikiendi hii itacheza mechi yake ya mwisho ya La Liga ikiwa tayari imeshalibeba taji hilo.
Real Madrid pia Juni Mosi itaumana na Borussia Dortmund katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wakati ikiwa katika mafanikio hayo, klabu hiyo inadaiwa kuwa katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wa mshambuliaji tishio duniani, Kylian Mbappe ambaye tayari ameshaaga katika timu yake ya sasa ya PSG.
“Kuogopa? Hapana. Ni kweli kwamba Mbappe ni mchezaji wa kipekee na kama atajiunga na Real Madrid, timu hiyo pamoja na mchezaji huyo wote watakuwa imara.
“Hata hivyo kwa mtazamo wetu ni kwamba haijalishi wachezaji ni wazuri kiasi gani, kama sisi tutakuwa pamoja kitimu, tukafanya kazi pamoja na kuwa na mtazamo sahihi, tunaweza kuwashinda, tunaweza kupambana nao,” alisema Lewandowski.
Lewandowski, 35, alijiunga na Barca Julai, 2022 na katika msimu wake wa kwanza aliisaidia timu hiyo kubeba taji la La Liga akiwa amefunga mabao 23.
Msimu huu hata hivyo umekuwa mgumu kwa timu hiyo pamoja na mshambuliaji huyo ingawa pamoja na hali hiyo ameweza kufunga mabao 18 ya ligi na kushika nafasi ya nne kwa kufunga mabao mengi.