Barcelona, Hispania
Rais wa Barcelona, Joan Laporta anatarajia kukutana na kocha wa klabu hiyo, Xavi Hernandez mapema wiki ijayo huku kukiwa na habari kwamba klabu hiyo inatafakari juu ya uamuzi wa kumuacha au kuendelea na kocha huyo.
Habari za ndani zinadai kwamba licha ya Xavi kutangaza mapema kwamba ataachana na timu hiyo baada ya msimu huu, uamuzi wa mwisho hadi sasa haujafikiwa na kumekuwa na sintofahamu kama aabaki au ataondoka.
Mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo, Deco na jopo la wasaidizi wake nao inatarajia watashiriki katika mkutano wa Xavi na Laporta ambao utafanyika baada ya mechi za mwisho za La Liga ambazo zitapigwa Jumapili ijayo.
Moja ya mambo ambayo imeelezwa kuwa yanatarajiwa kujadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na timu kumaliza msimu bila taji lakini pia mustakabali wa Xavi katika timu kama ataendelea kuwapo au wataachana naye.
Kwa kipindi kirefu zimekuwapo habari kwamba Laporta anamkubali Xavi na angependa aendelee kuinoa timu hiyo lakini baadhi ya wajumbe wa bodi wanaamini mabadiliko yanahitajika kwenye timu hiyo hasa baada ya kumaliza msimu bila taji.
Ikitokea Xavi akatimuliwa baadhi ya makocha wanaotajwa kuchukua nafasi yake ni Rafa Marquez wa timu ndogo ya Barca, Hans Flick, Thomas Tuchel, Thiago Motta na kocha wa zamani wa Brighton, Roberto De Zerbi.
Mapema mwezi uliopita zilikuwapo habari kwamba Xavi amebadili uamuzi wa kuachana na Barca na kwamba angeutumikia mkataba wake wa sasa hadi mwakani utakapofikia mwisho lakini kauli ya hivi karibuni ya kocha huyo kuhusu hali ngumu ya uchumi wa klabu hiyo huenda ikamponza.
Kimataifa Xavi, Rais Barca kufanya kikao
Xavi, Rais Barca kufanya kikao
Read also