Riyadh, Saudi Arabia
Kocha wa Al Hilal ya Saudi Arabia, Jorge Jesus amesema kwamba ana matumaini mshambuliaji wao, Neymar ambaye ni majeruhi atarudi mwezi Septemba na kuanza kuitumikia timu hiyo.
Neymar, 32, amekuwa nje ya uwanja tangu afanyiwe upasuaji wa goti la mguu wa kushoto baada ya kuumia wakati akiiwakilisha timu yake ya taifa ya Brazil, Oktoba mwaka jana.
“Kwa maumivu kama ya Neymar muda ambao wanautoa hadi mchezaji kupona ni kati ya miezi 10 hadi 11, tunadhani Neymar hatopona mwanzoni mwa msimu mpya, tunadhani kati ya Septemba au Oktoba atakuwa fiti,” alisema Jorge.
Baada ya kujiunga na Al Hilal akitokea PSG Agosti mwaka huu, Neymar ameichezea timu hiyo mechi tano tu kwenye Ligi Kuu Saudi Arabia kabla ya kuumia na hivyo kushindwa kuutumikia vizuri mkataba wake wa miaka miwili na timu hiyo.
Neymar ambaye ndiye anayeongoza kwa kuifungia timu ya taifa ya Brazil mabao mengi (mabao 79) pia atakosa kuiwakilisha Brazil kwenye michuano ya Copa America ingawa huenda akaiwakilisha kwenye mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026.
Wakati huo huo, Jorge naye amethibitisha kwamba yuko mbioni kuongeza mkataba na vinara hao wa Ligi Kuu Saudi Arabia akiwa anajivunia rekodi ya ushindi wa mechi 34 mfululizo akiwa na timu hiyo.
Kimataifa Kocha Al Hilal amsubiri Neymar
Kocha Al Hilal amsubiri Neymar
Read also